Jan 19, 2022 10:46 UTC
  • Mwakilishi wa Iran UN asifu maendeleo 'muhimu' ya kuwawezesha wanawake nchini licha ya vikwazo vya Marekani

Iran imepongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana hapa nchini katika kuwawezesha wanawake na wasichana, licha ya vikwazo vya Marekani vilivyo kinyume cha sheria na vya kinyama vinavyolenga nchi hiyo.

Balozi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, Majid Takht-Ravanchi ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichozungumzia suala la wanawake, amani na usalama.

Takht-Ravanchi amekumbusha jinsi vikwazo hivyo vinavyokiuka sheria za kimataifa na kukanyaga haki za kimsingi za wanawake na wasichana, haswa haki yao ya kupata maendeleo.

Amesema "licha ya vikwazo hivyo vya Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata maendeleo makubwa katika kuwawezesha wanawake na wasichana, hasa katika nyanja ya elimu."

Balozi wa kudumu wa Iran Umoja Mataifa ameongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu inatilia maanani sana nafasi ya wanawake katika maendeleo ya kijamii-kiuchumi na maisha ya kijamii-kisiasa ya jamii ya Iran."

Itakumbukwa kuwa, Marekani ilianza tena kutekeleza vikwazo hivyo mwaka 2018 baada ya kujiondoa kinyume cha sheria na kwa upande mmoja katika makubaliano ya nyuklia ya 2015 kati ya Iran na kundi la 5+1.

Washington imekataa kuondoa vikwazo hivyo hata vile vya vyakula na dawa, licha ya janga la virusi vya coona linaloendelea kuiathiri dunia.

Katika upande mwingine Majid Takht-Ravanchi amegusia hali ya wanawake katika eneo la Asia Magharibi, akielezea kusikitishwa kwake na athari mbaya za uvamizi na uingiliaji wa madola ya kigeni, pamoja na harakati za kigaidi zinazowalenga wasichana na wanawake katika eneo hilo. 

Amesema kesi kongwe zaidi ya uhalifu huo ni ya wanawake wa Kipalestina, ambao wanaendelea kuteseka kutokana na miongo kadhaa ya uvamizi wa Israel na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala huo haramu.

Tags