Jan 21, 2022 02:29 UTC
  • Mkutano wa marais wa Iran na Russia; nchi mbili zilizo katika mkondo wa pamoja wa kimkakati

Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran siku ya Jumatano alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Russia mjini Moscow ambapo pande mbili zimejadili masuala ya kieneo na kimataifa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Raisi ameashiria nafasi muhimu na yenye taathira ya Russia na Iran katika eneo na dunia na kusema: "Ufahamu wa pamoja wa nchi mbili kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa ni msingi wa ushirikiano wa pamoja. Uhusiano wa Russia na Iran uko katika mkondo wa pamoja wa kimkakati."

Aidha Raisi amesema kipaumbele katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa na maingiliano mema na nchi jirani na waitifaki na kuongeza kuwa, "kuimarishwa ushirikiano wa Iran na Russia kutapelekea kuboreka uchumi wa nchi mbili na pia kuimarika kiwango cha usalama wa kieneo na dunia nzima."

Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin wa Russia amesema hivi sasa kunatekelezwa miradi mikubwa ya maendeleo baina ya nchi mbili na kuongezwa kuwa Iran na Russia zinaendeleza ushirikiano katika nyanja mbali mbali. Ameendelea kusema: "Katika uga wa kimataifa, tuna ushirikiano wa karibu. Kwa jitihada za nchi hizi mbili, tumeweza kuisaidia Syria kukabiliana na magaidi wa kimataifa."

Mkutano wa marais wa Iran na Russia unajiri wakati ambao kumeshadidi mvuntano kati ya nchi za Magharibi na Russia hasa kuhusu Ukraine na hali kadhalika sambamba na mazungumzo ya Vienna ya kuondolewa vikwazo haramu dhidi ya Iran. Kwa hivyo mkutano wa Putin na Raisi una umuhimu mkubwa kwa mitazamo ya kiuchumi na kisiasa na ni mwanzo wa msimu mpya wa uhusiano baina ya nchi mbili kwa lengo la ushirikiano endelevu na wa muda mrefu.

Hivi sasa Iran na Russia zinakabiliwa na vikwazo haramu vya Marekani na zinapinga sera za Washington za upande mmoja na uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi zingine.

Iran na Russia zina maslahi ya pamoja ya kistratijia  katika uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiusalama. Aidha nchi hizi mbili zina mitazamo sawa katika masuala mengi ya kimataifa yakiwemo yale yanayojiri Asia ya Kati, Caucasia, Afghanistan, Yemen, Iraq na Syria katika vita dhidi ya ugaidi.

Ni kwa msingi huu ndio Iran na Russia sasa zinazingatia kwa kina uimarishwaji uhusiano wa pande zote hasa katika biashara, fedha, uwekezaji na ushirikiano wa muda mrefu katika miundomsingi ili kusambaratisha vikwazo.

Kuna maslahi mengi ya pamoja ya Iran na Russia na nchi mbili zinaweza kutumia uwezo wao mkubwa katika nyuga za mafuta na gesi na pia uchukuzi wa kimataifa kupitia korido ya kaskazini-kusini. Irada ya viongozi wa Iran na Russia katika kuimarisha ushirikiano katika nyuga zote unadhamini maslahi ya kiuchumi ya pande mbili na ni chanzo muhimu cha usalama na uthabiti katika eneo sambamba na kudhamini sera za kuhusishwa pande kadhaa katika masuala ya kimataifa.

Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Katika mkutano wa Raisi na Putin, kumefanyika mazungumzo mapana kuhusu masuala ya pande mbili, kieneo na kimataifa na hilo linaonyesha ukaribu wa mitazamo ya nchi hizi mbili na pia azma ya kuimarishwa uhusiano wa muda mrefu.

Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hivi kuhusu nukta hiyo: "Katika mkutano huu muhimu wa kirafiki na uliodumu kwa muda mrefu mjini Kremlin, Raisi na Putin wameainisha mkondo mpya na wa kasi katika uhusiano wa Tehran na Moscow. Katika msimu mpya wa uhusiano kutakuwa na uhusiano bora. Marais wa nchi mbili wamefikia mapatano ya kuainisha ramani mpya ya njia ya uhusiano wa muda mrefu."

Tags