Jan 21, 2022 03:18 UTC
  • Ebrahim Raisi: Siri ya kuwa Muislamu wa kweli ni kuijenga nafsi na kuwa mwema kwa wengine

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu amesema mbele ya Waislamu wa Msikiti Mkuu wa Moscow, mji mkuu wa Russia kwamba, Misikiti ni nyumba za Mwenyezi Mungu ardhini na inamlea vizuri Muislamu na jamii yake.

Ameongeza kuwa, mbali na Misikiti kuijenga vizuri nafsi ya mwanadamu na kuimarisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, nyumba hizo za Allah zinajenga na kuimarisha pia uhusiano mzuri wa kijamii wa Waislamu.

Rais Ebrahim Raisi amekwenda katika Msikiti Mkuu wa Moscow kwa mwaliko ya Mufti Mkuu wa Russia, Sheikh Rawil Gaynetdin na ameonana kwa karibu na Waislamu na kuzungumza nao.

Amesema, kuenea ufisadi na maadili maovu katika kila kona ya dunia leo hii ni ushahidi thabiti kwamba mwanadamu leo amemsahau Muumba wake. Amesema, miaka 70 imepita wananchi wa Palestina wanadhulumiwa na Wazayuni watenda jinai na zaidi ya miaka 20 wananchi wa Afghanistan waliishi chini ya uvamizi, ukatili na mauaji na hayo ni matunda ya siasa zisizo na maadili wala umaanawi.

Rais Ebrahim Raisi (kulia) akizungumza na Mufti Mkuu wa Russia, Sheikh Rawil Gaynetdin mjini Moscow

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia pia umuhimu wa Waislamu kushikamana vilivyo na mafundisho sahihi ya dini yao na kujiimarisha kiroho na kimaanawi akisisitiza kuwa, jinai zinazofanywa na magenge ya wakufurishaji katika nchi za Syria, Iraq, Afghanistan na Yemen tena kwa jina la Uislamu ni mambo ambayo hayana uhusiano wowote wa dini tukufu ya Uislamu bali ni njama za Markeani na Wazayuni ndizo zonazochochea na kuendesha jinai hizo.

Vile vile amesema, moja ya kazi muhimu za Misikiti katika Umma wa Kiislamu ni kuwaamsha Waislamu na kuzuia kuenea fikra za ukufurishaji na kwamba siri ya mtu kuwa Muislamu wa kweli ni kuimarisha nafsi yake na kuwatendea mema wengine.