Jan 21, 2022 13:24 UTC
  • Mkutano wa marais wa Iran na Russia waakisiwa na vyombo vingi vya habari vya Marekani

Mkutano na mazungumzo yaliyofanywa na marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia yameakisiwa mno na vyombo vya habari vya Marekani.

Shirika la habari la Associated Press limeandika: "Rais Vladimir Putin wa Russia alisema siku ya Jumatano alipokutana na Seyyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Moscow, kwamba angependa yafanyike mazungumzo ya kubainisha wasiwasi wa pamoja zilionao Russia na Iran kuhusu hali ya Afghanistan.

Rais wa Iran, naye pia amesema, Iran ina hamu ya kustawisha ushirikiano na Russia katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kiulinzi, kiusalama na ugunduzi wa anga za mbali.

Chaneli ya habari ya ABC News imesema, katika mazungumzo na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Vladimir Putin wa Russia amesifu na kupongeza ushirikiano wa nchi mbili katika masuala ya kimataifa ukiwemo mgogoro wa Syria.

Gazeti la New York Times limeandika: mkutano wa marais wa Iran na Russia unabainisha umoja wa nchi mbili katika kukabiliana na Marekani.

Gazeti hilo la Marekani limeongeza kuwa, katika mazungumzo na rais wa Russia, rais wa Iran amekumbusha kuwa, kwa muda wa miaka 40 sasa Tehran imesimama imara kukabiliana na Marekani.

Siku ya Jumatano, Seyyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliongoza ujumbe wa ngazi ya juu katika safari ya siku mbili nchini Russia, kufuatia mwaliko wa Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo.

Mbali na mazungumzo aliyofanya na mwenyeji wake, kuhudhuria na kuhutubia bunge la Duma, kukutana na Wairani wanaoishi Russia na kufanya kikao cha kubadilishana fikra na wadau wa sekta ya uchumi wa Russia ni miongoni mwa ratiba nyingine alizokuwa nazo rais wa Iran katika safari yake ya siku mbili nchini humo.../