Jan 22, 2022 14:10 UTC
  • Iran yalaani jinai za wavamizi wa Yemen dhidi ya raia wa kawaida

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali mashambulizi ya anga ya wavamizi wa Yemen katika makazi ya raia na kuua kwao kwa umati wananchi wa kawaida wasio na hatia.

Saeed Khatibzadeh amesema kuwa, mashambulio ya anga ya wavamizi wa Yemen ya siku kadhaa mfululizo katika maeneo ya raia na watu wa kawaida huko Yemen na jinai zao za kuteketeza mali za umma na kuua na kujeruhi kikatili makumi ya watu wasio na hatia ni jambo linalopaswa kulaaniwa na kila mwenye hisia za utu. Aidha ametumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa wafiwa na wahanga wote wa ukatili huo wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen.

Amesema, kuendelea mashambulio ya kijeshi katika maeneo ya makazi ya raia nchini Yemen kunachochewa na kimya cha jamii ya kimataifa na madola ya kibeberu yanayowapa wavamizi wa Yemen silaha za kila namna za kuangamiza raia. Aidha amesema matukio ya Yemen yanazidi kuthibitisha siasa za kindumilakuwili za madola ya kibeberu na wale wanaodai kupigania haki za binadamu ulimwenguni.

Saudia na watenda jinai wenzake hawawahurumii hata Waislamu misikitini 

 

Tayari harakati mbalimbali za Kiislamu kama Jihad al Islami ya Palestina na Hizbullah ya Lebanon zimelaani vikali jinai hizo za Saudi Arabia na wavamizi wenzake hasa Imarati huko Yemen.

Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Yemen Yahya Saree ameyashauri makampuni ya kigeni ya uwekezaji kuondoka Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kusema kuwa,  maadamu watawala wa Imarati wanaendelea na jinai zao dhidi ya Yemen, hii itakuwa na maana kwamba makampuni ya kigeni yaliyowekeza katika kijinchi hicho kidogo nayo hayatakuwa salama.