Jan 23, 2022 07:55 UTC
  • Mazoezi ya pili ya kijeshi baina ya Iran, Russia na China katika Bahari Hindi

Nchi za Iran, Russia na China, Ijumaa tarehe 21 Januari zilifanya mazoezi ya pili ya pamoja ya kijeshi katika eneo la kaskazini mwa Bahari Hindi chini ya kaulimbiu ya Mkanda wa Usalama wa Baraharini 2022.

Katika luteka na maneva hayo, majeshi ya nchi hizo tatu yalitumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushirikiana kuzima moto wa baharini, kuokoa chombo cha bahari kilichokuwa kimetekwa nyara, kushambulia maeneo maalumu pamoja na kufanya mashambulizi ya usiku dhidi ya vitu vya angani.

Vikosi vitatu vya majini vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, vikosi 11 vya Jeshi la Majini la Iran, vikosi vitatu vya jeshi la Russia na viwili vya Jeshi la Majini la China vilishiriki kwenye luteka na mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi.

Kuimarisha usalama wa biashara za bahari ya kimataifa, kupambana na maharamia na magaidi wa baharini, kubadilishana taarifa katika operesheni za uokoaji wa baharini, kubadilishana uzoefu wa kuendesha mbinu mbalimbali za kijeshi, ni miongoni mwa malengo ya luteka na mazoezi hayo ya kijeshi ya nchi tatu za Iran, China na Russia.

Admiral Mostafa Tajeddin

 

Admirali Mostafa Tajeddin, msemaji wa mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi ya baharini alisema kuwa, lengo la kufanyika luteka hiyo ni kuhakikisha nchi zote tatu za Iran, China na Russia zinafikia kiwango cha juu cha nguvu za kijeshi. Aliongeza kuwa: Leo hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nguvu za kutosha za kijeshi baharini kiasi kwamba ina uwezo wa kusimamia na kuongoza mazoezi ya kijeshi yanayoshirikisha madola makubwa ya kijeshi duniani.

Eneo yalipofanyika maneva ya Mkanda wa Usalama wa Baraharini 2022 yaani Bahari ya Hindi na Bahari ya Oman, ni eneo muhimu na la kiistratijia kwa nchi zote tatu za Iran, Russia na China. Eneo hilo lina njia kuu za baharini, lina malango bahari muhimu mno kama Bab al Mandab, Malaka na Hormuz na linahesabiwa kuwa ni pembe tatu za dhahabu kutokana na umuhimu wake mkubwa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana majeshi ya majini ya nchi tatu za Iran, China na Russia zikaamua kuanzisha mazoezi ya pamoja ya baharini katika eneo hilo tangu mwaka 2019.

Bahari ya Oman na ukanda wa kaskazini mwa Bahari Hindi ni miongoni mwa maeneo muhimu mno na yanayotegemewa sana katika safari za biashara duniani. Sehemu kubwa ya biadhaa za mafuta na zinazotokana na mafuta za Iran zinasafirishwa kwa njia ya bahari. Biashara ya kimataifa ya Russia pamoja na mafuta yanayotumika nchini China na biashara nyingi za nchi hiyo zinafanyika kwa njia ya safari za baharini. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za China na Russia zinafanya juhudi za kulinda kwa pamoja usalama wa eneo hilo muhimu zaidi la safari za baharini katika ukanda huu ili kuhakikisha manufaa yao hayahatarishwi kivyovyote vile.

Sehemu ya mazoezi ya kijeshi ya nchi tatu za Iran, China na Russia ya Mkanda wa Usalama wa Baraharini 2022 yaliyofanyika kaskazini mwa Bahari Hindi

 

Ni jambo lililo wazi kwamba, kushiriki bega kwa bega Iran katika mazoezi kama hayo ya kijeshi na madola makubwa kama China na Russia ni ushahidi mwingine kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijatengwa licha ya vikwazo vikubwa vya kidhulma ilivyowekewa na Marekani. Vile vile linabainisha kuwa, nafasi na hadhi ya Iran kimataifa ni kubwa.

Kufanyika mazoezi ya kijeshi ya Mkanda wa Usalama wa Baraharini 2022 pia kunaweza kuwa na ujumbe kwamba madola ajinabi ambayo ndio wasababishaji wakuu wa ukosefu wa usalama katika eneo hili yanapaswa kutambua kwamba, suala la kulinda utulivu, usalama na amani ya eneo hili linapewa umuhimu mkubwa na nchi hizo tatu hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Song Zhongping, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijeshi raia wa China anasema kuhusu luteka hiyo kwamba: Nchi tatu za Iran, China na Russia lazima ziongeze kiwango cha ushirikiano wao katika nyuga mpya za kiusalama hususan katika masuala ya usalama wa safari za baharini kwani hivi sasa baadhi ya nchi zinafanya usumbufu baharini licha ya kwamba huo ni uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Usalama wa safari za kimataifa za baharini ni muhimu sana kwa nchi hizo tatu.