Jan 24, 2022 12:09 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Ishara za jamii inayofuata kigezo cha Fatima Zahra SA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema huduma bila kujigamba na kwa ikhlasi kwa wanaohitaji ni moja ya ishara muhimu za jamii inayofuata kigezo cha Fatima Zahra SA.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, alisema hayo Jumapili mbele ya hadhara ya wasomaji wa tungo za kuwasifu Ahlul-Bayt wa Mtume SAW kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuzaliwa Bibi Fatima SA, binti ya Mtume Muhammad SAW.

Katika kikao hicho Kiongozi Muadhamu amebainisha mitazaamo kuhusu shakhsia ya Bibi Fatima Zahra kama vile harakati za kijamii na kutoa huduma kwa ikhlasi bila kujigamba na kusema kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, jamii ya Iran imekuwa ni jamii yenye kumfuata Fatima Zahra SA kama kigezo.

Kutoa huduma za uhakika na zenye ilkhlasi kwa wanaohitajia ikiwemo kukidhi mahitaji ya wale wasioweza kujimudu katika mahitaji ya kimsingi kabisa ni jambo ambalo linasisitizwa sana katika Qur'ani Tukufu na pia katika hadithi na riwaya za Kiislamu na jambo hilo limeweza kudhihirika wazi katika jamii ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kuna mifano mingi ya aina yake katika jamii ya Kiislamu ya Iran na mojawapo ya mifano huyo ni miaka minane ya kujitolea watu wa Iran ya Kiislamu katika zama za kujihami kutakatifu na katika zama hizi kujitolea wafanyakazi wa sekta ya afya katika kukabiliana na kirusi angamizi cha corona. 

Katika kujitolea muhanga huko, nafasi ya wanawake ni muhimu na yenye kutiliwa maanani. Wafanyakazi wa sekta ya afya, hasa wauguzi na madaktari kinamama na wanawake pambizoni mwa shughuli zao za kifamilia wamekuwa wakifanya kazi kwa ikhlasi katika sekta ya tiba na hata baadhi wamekufa shahidi wakiwa kazini. Huu ni mfano wa wazi wa jamii inayomfuata Bibi Fatima Zahra SA kama kigezo.

Wanawake Wairani wauguzi wakiwa hospitalini wakati wa janga la COVID-19

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, wanawake na mabinti wa Iran ambao Fatima Zahra SA ni kigezo chao katika mkondo wa ukamilifu maishani, sawa na walivyofanya katika uga wa utamaduni wakati za zama za kujihami kutakatifu, wamekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na janga la corona kwa ikhlasi na kwa mapenzi ya mama. Kwa kujitolea kwao, wanawake Wairani wameweka ukurasa mpya na wa kudumu katika jamii ya Iran ya Kiislamu ambayo inafuata kigezo cha Bibi Fatima Zahra SA.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita wanawake wauguzi Wairani wamekuwa wakikaa mbali na wazazi, watoto na waume zao  ili kuwahudumia  na kuwaokoa wagonjwa kijihadi katika hospitali bila kujali rangi, kaumu na utamaduni.

Waziri wa Afya wa Iran Daktari Ainullahi akizungumza Jumapili kwa mnasaba wa Siku ya Mama na Siku ya Mwanamke Iran alisema: "Wanawake wamekuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na janga la COVID-19.  Wanawake katika sekta ya afya wamefanya kazi kwa ukarimu na subira na wamekuwa na nafasi muhimu katika kunusuru maisha ya watu katika Jamuri ya Kiislamu ya Iran."

Ukarimu wa mwanawake Wairani umeng'ara kama mbalamwezi duniani, huyu ni mama na mwanamke ambaye katika zama za vita vya Iraq dhidi ya Iran, wakati ambao ni maarufu kama zama za kujihami kujitakatifu, alitumia suhula za awali kabisa kutoa huduma katika mstari wa mbele wa vita na hayo yote yalifanyika ikiwa ni katika kuiga mafundisho ya Bibi Fatima Zahra SA. Kujitolea katika zama hizo kulikuwa mfano wa kuigwa na kizazi kipya cha Mapinduzi ya Kiislamu.

Kama alivyosema Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, "Bibi Fatima Zahra SA anapaswa kuwa kigezo katika nyuga zote hasa harakati za kijamii na kimapinduzi."