Jan 24, 2022 14:06 UTC
  • Rais Ebrahim Raisi: Uhusiano wa Iran na nchi za Afrika utaimarishwa zaidi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao chake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo kuwa: Suala la kuimarishwa uhusiano wa Iran na nchi za bara la Afrika litafuatiliwa kwa umakini na nguvu zaidi.

Rais wa Iran Sayyid Ebrahim Raisi leo (Jumatatu) amesema wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo, Robert Dussey, kwamba nchi za Afrika zina utajiri mkubwa wa madini nguvukazi na vipawa na kuongeza kuwa, "Tehran inataka kuimarisha uhusiano wa pande zote na nchi za Kiafrika ikiwa ni pamoja na Togo kwa ajili ya maslahi ya pamoja ya mataifa yote.

Rais Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa, "katika kipindi chote cha historia Wamagharibi wamekuwa wakitaka kuzikoloni na kuzinyonya nchi za bara la Afrika, na leo hii wanaendelea kufuatilia maslahi na malengo yao katika bara hilo kwa njia mbalimbali". Vilevile amepongeza juhudi za watu wa Afrika za kulinda uhuru na kujitawala kwa nchi zao na akasema mafanikio ya nchi hizo yamo katika kulinda utambulisho wao wa kitaifa na kitamaduni na kuendelea kusimama kidete. 

Raisi akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo

Rais wa Iran amesema: "Nchi za Kiafrika zina uwezo unaohitajika kwa ajili ya maendeleo na ustawi, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono uhuru, maendeleo na ustawi wa watu wa Afrika."

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo amesisitiza kuwa, nchi hiyo inataka kuanzisha uhusiano mpana na wa pande zote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, Lome ina matumaini na mwenendo wa Tehran wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Afrika.

Akilaani vikwazo vikali vya nchi za Magharibi dhidi ya nchi na mataifa huru, Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo amesisitiza kuwa: "Tunataka ushirikiano wa pamoja na Iran."

Tags