Jan 25, 2022 02:39 UTC
  • Ebrahim Raisi: Iran inapigania kuwa na uhusiano bora na nchi jirani na za Waislamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran muda wote inalipa umuhimu mkubwa suala la kuimarisha uhusiano wake na nchi jirani hasa zile za Waislamu.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo wakati alipokuwa anapokea vitambulisho vya Ismail Abdul Manaf, balozi mpya ya Brunei hapa mjini Tehran jana Jumatatu na kusema kuwa, uhusiano wa nchi hizi mbili za Waislamu unatokana na uhusiano imara na wa ndani ya nyoyo za watu wa nchi hizi mbili na kwamba kuna udharura wa kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara wa Iran na Brunei.

Rais Raisi pia amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa umuhimu mkubwa suala la kuimarisha uhusiano wake na nchi zote duniani na hasa nchi jirani na za Waislamu.

Bendera za Iran na Brunei

 

Amesema, ni matumaini yetu ushirikiano na miamala ya kirafiki na kidugu baina ya nchi mbili baina ya Iran na Brunei unazidi kuimarika zaidi na zaidi katika upeo wa kieneo na kimataifa.

Naye Ismail Abdul Manaf, balozi mpya wa Brunei hapa mjini Tehran amefikisha salamu za Mfalme wa Brunei, al Haj Sultan Hassanal Bolkiah kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kwamba, akiwa balozi mpya wa Brunei hapa Tehran atafanya juhudi zake zote kuhakikisha uhusiano baina ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaimarika kikamilifu, kadiri inavyowezekana na katika nyuga zote.