Jan 25, 2022 08:05 UTC
  • Iran: Hatujaamua kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani

Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haijafikia uamuzi wa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumatatu hapa mjini Tehran, akizungumza na waandishi wa habari pambizoni mwa Kongamano la Kitaifa la Majirani na kueleza kuwa, Wamarekani wanaendelea kuiomba Iran ifanye mazungumzo ya moja kwa moja nao, lakini Tehran haijafanya uamuzi wowote kuhusu kadhia hiyo kwa sasa.

Ameeleza bayana kuwa: Kwa sasa mazungumzo Vienna kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanafanyika katika ngazi za wataalamu waandamizi, wakurugenzi wa masuala ya siasa, na manaibu mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la 4+1.

Mkutano wa Vienna

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amesema ni matumaini ya Jamhuri ya Kiislamu kuwa kilele cha mchakato mkuu wa mazungumzo ya Vienna kitafikiwa pasi na kuwashirikisha viongozi wa ngazi za juu.

Haya yanajiri wakati huu ambapo Marekani inashiriki kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwenye duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna, ambayo ajenda yake kuu ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na visivyo vya kisheria ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inayoendelea tokea mwishoni mwa mwaka jana 2021.

Tags