Jan 25, 2022 12:31 UTC
  • Sisitizo la Rais wa Iran la kupanua uhusiano na majirani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran imekuwa ikifuatilia suala la kuimarisha uhusiano wake na nchi jirani hasa zile za Waislamu.

Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana wakati alipokuwa anapokea vitambulisho vya Ismail Abdul Manaf, balozi mpya ya Brunei hapa mjini Tehran na kusema kuwa, uhusiano wa nchi hizi mbili za Waislamu unatokana na uhusiano imara na wa ndani ya nyoyo za watu wa nchi hizi mbili na kwamba, kuna udharura wa kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara wa Iran na Brunei. Tangu serikali ya awamu ya 13 ilipoanza kazi zake Agosti 3 mwaka jana (2021) imeonyesha kuwa, inaaamini suala la uwiano katika sera za kigeni na imekuwa ikitoa kipaumbele katika sera zake juu ya suala la kupanua ushirikiano na majirani pamoja na mataifa ya Waislamu.

Aidiolojia ya kuweko uwiano katika sera za kigeni katika serikali ya awamu ya 13 ya Iran sambamba na kuzingatia na kutilia mkazo uhusiano na madola makubwa ya mashariki na magharibi, inafuatilia kadhia ya kupinga kuwa na mielekeo ya Umagharibi mtupu katika mahusaino ya kigeni. Sayyid Ebrahim Raisi aliashiria katika hafla ya kuapishwa kwake iliyofanyika katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran juu ya kuibuka mageuzi katika ulimwengu wa sasa na kusisitiza kwamba, kudhamini maslahi ya mataifa kunafungamana na kudiriki ulimwengu mpya na ushirikiano wa kistratejia na madola makubwa yanayochomoza na siasa za kigeni mwafaka na zenye uwiano.

Siasa za muelekeo wa kieneo, mtazamo wa kuelekea mashariki, kushiriki katika asasi na jumuiya za kieneo na nje ya eneo kama Jumuiya ya Shanghai na Jumuiyya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) ni miongoni mwa misdaqi na mifano ya wazi ya kuleta uwiano katika sera za kigeni za Iran zinazofuatiliwa na kutekelezwa na serikali ya awamu ya 13 ya Iran inayoongozwa na Rais Ebrahim Raisi.

Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran

 

Miongoni mwa sifa maalumu za sera za kigeni za Iran zenye uwiano ni kwamba, sambamba na na kuzingatia vipaumbele zinatumia fursa pia katika nyuga nyingine ulimwenguni kwa ajili ya  kudhamini kwa kiwango cha juu kabisa maslahi ya kitaifa. Mazungumzo na mashauriano ya Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wenzake wa Ulaya katika safari yake huko New York na vilevile mazungumzo ya Iran na kundi la 4+1 linaloundwa na mataifa ya Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusiana na kuondolewa vikwazo Iran ni miongoni mwa hatua za serikali ya awamu ya 13 katika mkondo wa kuleta uwiano katika sera za kigeni.

Abdollahian anasema kuhusiana na  hilo kwamba, kufanya mazungumzo na mashauriano na Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa mataifa 18 ya Ulaya ni ishara ya wazi kwamba, sera za mtazamo kwa mashariki haina maana ya kuuweka kando kikamilifu ulimwengu wa Magharibi.

Filahi kunashuhudiwa machafuuko na hali ya mchafugoke katika baadhi ya mataifa ya Asia na Marekani nayo imelazimika kuondoka katika eneo hili la Asia Magharibi; kwa msingi huo kuna haja ya kuweko mtazamo mmoja wa mataifa ya eneo ambayo kikawaida ni mataifa ya Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na vitisho na wakati huo huo kuandaa fursa za kiuchumi kwa ajili ya kudhamini maslahi yya mataifa na kulipa umuhimu hilo kuliko ilivyokuwa hapo kabla.

Ebrahhim Raisi, Rais wa serikali ya awamu ya 13 ya Iran

 

Kuhusiana na suala hilo, Serikali ya Awamu ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kufuatilia suala la kuimarisha uhusiano majirani na mataifa ya Waislamu na diplomasia ya kiuchumi imekuwa ikifanya hima pia ya kuongeza mahusiano na mashirikiano ya kibiashara na mataifa hayo. Utendaji huu umepelekea kupungua mizozo na hitilafu katika eneo.

Safari ya hivi karibuni ya Rais Ebrahim Raisi nchini Takjikistan na uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Shanghai, safari ya kuelekea Turkemanistan na kushiriki katika kikao cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO), safari yake nchini Russia na kuandaliwa utangulizi wa kutiwa saini hati ya ushirikiano wa miaka 20 na taifa hilo, kuchorwa ramani ya njia ya uhusiano wa Baku na Tehran na kadhalika safari za kieneo za Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika eneo zinahesabiwa kuwa ni miongoni mwa hatua chanya za Serikali ya Awamu ya 13 zenye lengo kutekeleza siasa za ujirani mwema na kutoa kipaumbe katikka uhusiano wake na mataifa jirani.