Jan 27, 2022 02:35 UTC
  • Mazungumzo ya Vienna; ufunguo wa makubaliano yoyote ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi ameeleza kuwa, ufunguo wa mapatano yoyote ya kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya wananchi wa Iran.

Rais Ebrahim Raisi ameyasema hayo baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuchapisha tafsiri mbalimbali za uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Iran na Marekani kuhusu makubaliano ya kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA.  

Duru mpya ya mazungumzo ya kuhuisha mapatano ya JCPOA inaendelea mjini Vienna kwa lengo kuu la kuondolewa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya wananchi wa Iran, na ripoti chanya zimechapishwa kuhusu maendeleo ya mazungumzo hayo na mikutano ya kuandika matini yake ya mwisho. Sambamba na mazungmzo hayo kumetolewa baadhi ya habari na maoni, ikiwa ni pamoja na pendekezo la kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran ili kufikia makubaliano ya kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika mazungumzo yake ya moja kwa moja ya televisheni na wananchi Jumanne ya jana, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ebrahim Raisi aligusia mchakato wa hivi karibuni wa mazungumzo ya Vienna na msimamo wa Iran kuhusu ombi la Marekani la kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Iran na kusema: Ombi hili si jipya na limetolewa kwa muda mrefu, lakini hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika na Wamarekani.

Sayyid Ebrahim Raisi

Hatua yoyote mpya ya kutayarisha njia ya kufikia makubaliano ya kufufua JCPOA inapaswa kuoanisha baina ya maneno na vitendo halisi, na hapana shaka kuwa matamshi yanayotolewa na baadhi yana madhumuni maalumu na kwa ajili ya kuathiri vyombo vya habari. Vilevile kuna umhimu wa kuelewa kwamba hali ya kuaminiana inapatikana kwa mienendo sahihi na ya kweli na si maneno matupu. Uzoefu wa mapatano ya JCPOA unaonyesha kuwa, mienendo ya Wamarekani inatofautiana na kwenda kinyume na maneno yao. Barack Obama alitia saini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2015, lakini Marekani ya Trump ilijiondoa kwenye mapatano hayo mwaka 2018 na kuweka vikwazo vipya dhidi ya watu wa Iran.

Hivyo basi ili kujenga hali ya kuaminiana kuna ulazima wa kuwepo uwiano baina ya maneno na matendo ya pande zote wanachama wa mapatano ya JCPOA hususan Marekani. Iwapo hili litatimia na kuthibitishwa na Jamhuri ya Kiislamu, kutakuwepo matumaini makubwa ya kupigwa hatua mpya ya kufikiwa mapatano mazuri katika mazungumzo ya Vienna.

Hata hivyo hali ya sasa katika mazungumzo hayo ni kwamba njia ya mawasiliano kati ya Iran na Marekani ni ya kutuma na kupokea maoni ya maandishi, na hadi kutakapokuwepo yakini kwamba mazungumzo ya moja kwa moja baina ya pande mbili yanaweza kuleta tija na kusababisha makubaliano mazuri, Iran haioni udharura wa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.

Katika hali hiyo, Jamhuri ya Kiislamu bado haijachukua uamuzi mpya kuhusu pendekezo la Marekani la kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani mjini Vienna.

Mazungumzo ya Vienna 

Iran haitaki mikutano na mazungumzo ya kimaonyesho na mkondo wa hivi sasa wa mazungumzo ya Vienna hautabadilika hadi pale kutakapokuwepo irada na azma ya kweli ya kuondoa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya wananchi wa Iran na kisha kudhamini uhakiki wa kupata maslahi ya kiuchumi ya Iran.

Kama alivyosema Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, hadi sasa mawasiliano na ujumbe wa Marekani mjini Vienna yamefanyika kwa kubadilishana maandishi yasiyo rasmi, na njia hii itabadilishwa na mbinu nyingine pale tu makubaliano mazuri yatakapopatikana.

Tags