Jan 27, 2022 07:59 UTC
  • Iran yajibu uropokaji wa Uingereza kuhusu mazungumzo ya JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali bwabwaja mpya zilizotolewa na Uingereza juu ya mazungumzo ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanayoendelea huko Vienna, Austria.

Saeed Khatibzadeh ameyataja kuwa ya kipumbavu na yasiyo na msingi matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza aliyedai kuwa, Iran itabeba dhima kwa mkwamo wowote utakaojitokeza kwenye mazungumzo hayo, ambayo lengo lake kuu ni kuondolewa Tehran vikwazo haramu.

Siku ya Jumanne, Liz Truss, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza alitoa kauli ya uropokaji akidai kuwa, iwapo mazungumzo hayo yatagonga mwamba eti kutokana na ukwamishaji wa Iran, basi machaguo yote yapo mezani.

Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, kauli hiyo Truss ni karata nyingine ya mchezo wa lawama wa Wamagharibi, ili kujaribu kuficha kushindwa kwao kuchukua hatua zozote za kuyanusuru mapatano hayo, wakati Marekani ilipojiondoa kwayo mwaka 2018.

 Liz Truss, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza

Khatibzadeh amesema nchi za Ulaya si tu hazikuchukua hatua za maana za kuiokoa JCPOA, lakini zilienda mbali zaidi na kuunga mkono vikwazo haramu na vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya taifa la Iran.

Iran inasisitiza kuwa, endapo pande husika katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zitakuwa tayari kuliondolea vikwazo vya kidhalimu taifa hili, basi kuna uwezekano wa kufikiwa aina yoyote ya makubaliano kamili.

Tags