Jan 28, 2022 08:24 UTC
  • Umuhimu wa safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar mjini Tehran

Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo siku ya Alhamisi alifanya ziara mjini Tehran ambapo alionana na kuzungumza na waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Iran Hussein Amir Abdollahian.

Safari hiyo imefanyika katika hali ambayo mawaziri hao wa mambo ya nje Jumanne usiku walizungumza kwa njia ya simu ambapo walijadili na kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa pande mbili na masuala ya kieneo.

Suala la mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 4+1 pia limepewa uzito katika mazungumzo hayo. Mazungumzo hayo ya nyuklia yanaendelea mjini Vienna Austria ambapo Marekani inashiriki kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Akizungunza Jumatatu katika kikao cha kufunga maonyesho ya kitaifa ya Iran na nchi jirani kilichofanyika katika Kituo cha Utafiti wa Kisiasa na Kimataifa cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Hussein Amir Abdollahian alisema: "Iwapo kufikiwa makubaliano mazuri na yaliyo na dhamana ya juu kutahitajia mazungumzo na Wamarekani, hatutapuuza suala hilo." Katika mazungumzo ya moja kwa moja na wananchi Jumanne usiku, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hakufutilia mbali uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani, na kushurutisha suala hilo na kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran. Alisema: “Hadi sasa hatujafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani. Ikiwa upande wa pili uko tayari kuondoa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya watu wa Iran, kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano yoyote."

Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani (kushoto) na Amir Abdollahian mjini Tehran

Matamshi hayo yalikaribishwa na viongozi wa Marekani. "Washington iko tayari kwa mazungumzo ya moja kwa moja na ya haraka na Iran ili kuendeleza mazungumzo ya nyuklia," msemaji wa White House Jen Saki aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu jioni katika kujibu matamshi ya Amir Abdollahian. Kwa kuzingatia masuala hayo, inaonekana kwamba Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amebeba ujumbe kutoka kwa Wamarekani kwenda Iran na wakati huohuo kujaribu kuhuisha siasa za jadi za Qatar, ambazo ni za kupatanisha mataifa tofauti ya dunia. Kabla ya hapo, kwa mara kadhaa Qatar iliwahi kuwa mpatanishi kati ya Tehran na Washington au kuwasilisha jumbe za pande zote mbili.

Aidha, vita vya Yemen ni moja ya masuala muhimu katika eneo, na huenda mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizi mbili walijadiliana kuyahusu. Katika siku za karibuni, mashambulizi ya muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen yameongezeka na raia wengi wamekuwa wahanga wa mashambulizi hayo. Kuhusu hilo Hussein Amir Abdollahian amesema: "Katika wiki za karibuni, kumekuwa na ongezeko la shughuli za kijeshi nchini Yemen, ambazo zimechochea vita nchini Yemen na katika eneo, na hivyo kuharibu njia ya amani."  Mohammed bin Abdulrahman al-Thani naye kwa upande wake amesema nchi yake ina wasi wasi juu ya kuongezeka mivutano mipya katika eneo na kwamba inaamini kuwa hakuna suluhu ya kijeshi kwa mgogoro wa Yemen bali unapaswa kutafutiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo, na kwamba hali ya sasa haina maslahi kwa upande wowote ule.

Uhusiano wa pande mbili kati ya Qatar na Iran pia ni miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele katika mazungumzo ya Amir Abdollahian na Mohammad bin Abdulrahman. Qatar ni miongoni mwa nchi ambazo zina uhusiano mzuri na Iran na daima  nchi mbili hizi zimekuwa na ujirani mwema na uhusiano wa amani. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha mvutano wa ndani ya nchi za Kiarabu uliodumu kwa miaka minne kati ya Qatar na nchi nne za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri, ililaani uingiliaji wao wa masuala ya ndani ya Qatar na kuiunga mkono kikamilifu katika kukabiliana na hali hiyo ya vitisho.

Safari ya Abdulrahman Al-Thani mjini Tehran

Mazungumzo ya kidiplomasia pia yamekuwa yakiendelea kati ya nchi mbili hizi. Hivi karibuni Amir Abdollahian alisafiri hadi Oman na Qatar na kukutana na viongozi wa nchi hizo. Katika kikao na Amir Abdollahian tarehe 11 Januari, Mohammad bin Abdulrahman, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alieleza nia ya nchi hiyo ya kupanua ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika uwanja wa kiuchumi. Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa moja ya malengo ya safari ya Alhamisi ya Mohammad bin Abdulrahman mjini Tehran ilikuwa ni kudhihirishwa hamu ya pande mbili kwa ajili ya kupanua uhusiano wao katika nyanja tofauti.

Tags