Jan 29, 2022 02:59 UTC
  • Maandamano ya kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Yemen yafanyika nchini Iran

Maelfu ya wananchi katika miji mingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameshiriki katika maandamano ya kuunga mkono taifa linalodhulumiwa la Yemen na kulaani jinai zinazotendwa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudia dhidi ya taifa hilo.

Mjini Tehran baada ya Sala ya Ijumaa katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA, maelfu ya waumini walishiriki katika maandamano ya kuunga mkono taifa la Yemen.

Waandamanaji walisikika wakitoa nara kama vile 'Mauti kwa Marekani'. 'Mauti kwa Wazayuni na Mawahabi Waibua Fitina Kubwa'. 'Mauti kwa Aal Saud', na "Kimya Mbele ya Jinai ni Usaliti'. Aidha waandamanaji walitoa nara ya kuunga mkono taifa la Yemen kwa kusema 'Salamu kwa Watu wa Yemen'. 

Siku za karibuni maeneo ya makazi ya raia nchini Yemen yamekuwa yakilengwa zaidi kwa mashambulizi makali ya anga ya ndege za kivita za Saudia ambapo mamia ya raia wameuawa au kujeruhiwa, wengi wakiwa ni wanawake na watoto. Jumanne iliyopita ndege za kivita za Saudia zilishambulia mkoa wa kaskazini mwa Yemen wa Sa'ada na kuua watu 91. Watu wengine wasiopungua 236 walijeruhiwa. Waziri wa Afya wa Yemen Al-Mutawakil amesema muungano wa vita unaoongozwa na Saudia unalenga waziwazi na kuwaua makusudi raia wasio na hatia. 

Maandamano baada ya Sala ya Ijumaa Tehran kuunga mkono Wayemen na kulaani muungano vamizi wa Saudia ambao unapata himaya ya Marekani, utawala haramu wa Israel na Uingereza katika jinai dhidi ya Wayemen

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesisitiza kuwa, mauaji ya jela ya Saada nchini Yemen yalitekelezwa kwa silaha za Marekani kufuatia mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudi Arabia.

Ripoti hiyo imesema: "Muungano vamizi wa Saudia ulifanya mashambulizi makubwa ya anga kaskazini mwa Yemen, ikiwa ni pamoja na katika mji wa Sana'a, katika wiki iliyopita, na kuua makumi ya raia na kuharibu miundombinu na vituo vya huduma za kijamii."

Marekani na utawala haramu wa Israel ni washirika wakuu wa Saudi Arabia na Imarati katika vita dhidi ya taifa la Yemen. 

Tags