Jan 31, 2022 04:01 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; ushindi wa ngome ya uzalishaji katika vita vya kiuchumi vya adui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kusimama kidete sekta ya uzalishaji bidhaa za ndani mbele ya hujuma za kiuchumi na njama za adui za kujaribu kuizuia Iran isiuze mafuta na gesi yake, na pia kusimama imara mbele ya vita vya kuifungia Tehran vyanzo vya fedha za kigeni na kupanga njama za kuzuia mabadilishano ya kibiashara ya Iran na nchi nyingine, kwa hakika ni jihadi na ni miongoni mwa ibada kubwa kabisa.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, alisema hayo jana Jumapili mbele ya wamiliki wa viwanda na wazalishaji wa bidhaa za ndani ya Iran na kusisitiza kuwa, njama za adui za kujaribu kuishinda ngome ya uzalishaji bidhaa za Iran zimefeli. Amesema: Katika hujuma hiyo dhidi ya uchumi wa nchi yetu, maisha wananchi yamekumbwa na matatizo lakini uchumi wa Iran haukupigishwa magoti; kiasi kwamba, siku chache nyuma msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alitangaza wazi kuwa sera ya mashinikizo ya juu kabisa imepelekea Marekani kushindwa kifedheha.

Ustawi wa kiuchumi na uzalishaji wa bidhaa ni miongoni mwa vielelezo vya kuwa na nguvu za kiuchumi nchi na taifa. Wakati huu ambapo vita vya klasiki havina maana maalumu, suala la kuimarisha nguvu za kiuchumi na kufanya mapinduzi katika uzalishaji wa bidhaa za ndani lina umuhimu mkubwa katika muqawama na kusimama imara kupambana na mbinu mpya za mashambulizi ya adui.

Tangu katika miaka ya mwanza kabisa ya umri wa Jamhuri ya Kiislamu, maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu walianzisha vita vya kijeshi ili kuzuia maendeleo ya mapinduzi machanga ya wananchi wa Iran na walielekeza mashambulizi yao katika pembe zote zilizotia nguvu mapinduzi hayo. Lakini njama hizo zimeshindwa; na walipoona zimeshindwa, waliamua kutumia mbinu nyingine kukabiliana na taifa la Iran.

 

 

Vikwazo na "mashinikizo ya kiwango cha juu" ni silaha mbili mpya zilizotumiwa na maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu ili kwa kuongeza mashanikizo dhidi ya uchumi wa Iran, waweze kukwamisha kikamilifu harakati za uzalishaji bidhaa ndani ya Iran na baadaye mfumuko usiodhibitika wa bei uingie kwenye uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ili hatimaye wananchi wasimame kuupinga mfumo wa Kiislamu humu nchini. Lakini pamoja na kuwepo matatizo mbalimbali ya kila namna, gurudumu la uzalishaji bidhaa la Iran limeendelea kuzunguka wakati wa kivuli kikubwa cha mashinikizo ya kiwango cha juu na vikwazo vya kidhulma na kufanikiwa kufelisha njama za adui.

Wakati janga la corona lilipoikumba dunia, hali ya kupatikana bidhaa muhimu na za kimsingi za watu ilikuwa mbaya katika baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani, lakini nchini Iran bidhaa muhimu za wananchi ziliendelea kupatikana kama kawaida na hazikukumbwa na changamoto kama zilizowakumbwa wananchi wa baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani. Hilo lilitokana na msingi imara uliojengewa uchumi wa Iran. 

Katika siku na miezi ya awali ya kuenea ugonjwa wa UVIKO-19 yaani corona, nchi nyingi duniani zilishindwa kupata vifaa vya tiba vya kukabiliana na janga hilo na zililazimika kuagizia vifaa hivyo kutoka nje. Lakini Iran kutokana na kuwa na msingi imara wa uzalishaji wa bidhaa za matibabu pamoja na ubunifu wa wanasayansi wake, mashirika ya taifa hili la Kiislamu yalifanikiwa kuzalishaji haraka vifaa vya tiba vya kutibu ugonjwa wa corona vikiwemo vya kuwasaidia kupumua wagonjwa wa corona na vya kuchukulia vipimo vya ugonjwa huo.

Uchumi wa kimuqawama 

 

Uzalishaji bidhaa katika sekta nyingine za viwanda za Iran pia hali yake ni ya kuridhisha kabisa. Leo hii uzalishaji wa bidhaa za pertokemikali, sekta ya feleji, madini na sekta nyingine unatoa mshango muhimu katika kuimarisha ngome ya uzalishaji vidhaa na uchumi wa Iran. Kwa mfano, sekta ya bidhaa za petrokemikali  ina umuhimu mkubwa mkubwa katika uingizaji wa fedha za kigeni humu nchini. Kwa kutegemea wanasayansi wa ndani ya Iran, sekta hiyo haikutetereka hata wakati vikwazo vya adui vilipokuwa vimepamba moto. Katika kipindi hicho cha mashinikizo ya hali ya juu, sekta hiyo ilifanikiwa kusafirisha nje ya Iran bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 9, yaani thuluthi nzima ya fedha za kigeni zilizohitajiwa na Iran.

Huo ni uthibitisho wa kivitendo wa ubora wa sera za Jamhuri ya Kiislamu za uchumi wa kimuqawama wa kutegemea uzalishaji wa ndani ya nchi na ubunifu wa kiteknolojia wa wasomi wa Iran. Kwa kweli uchumi wa namna hiyo wa kimuqawama ndilo suluhisho bora la uchumi usiotetereshwa na misukosuko inayotokea kila leo duniani. Uzalishaji wa bidhaa bora za ndani ya nchi ni ngao na kinga kwa uchumi wa Iran mbele ya mashambulio ya kila upande ya adui.

Tags