Feb 03, 2022 12:56 UTC
  • Abdollahian: Iran yataka kufikiwa makubaliano ya kudumu na ya kutegemewa Vienna

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kufikia makubaliano ya kudumu na ya kutegemewa baina yake na kundi la 4+1 katika mazungumzo ya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA huko Vienna, Austria.

Hossein Amir Abdollahian ameyasema hayo leo Alkhamisi katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Japan, Hayashi Yoshimasa na kuongeza kuwa, Iran ina azma ya kweli ya kufikiwa makubaliano mazuri, ya kudumu na ya kutegemewa kwenye mazungumzo hayo ya Vienna.

Aidha ameishukuru Japan kwa jitihada zake za kutaka kuona makubaliano yanafikiwa kwenye mazungumzo hayo ya Vienna, ambayo lengo lake kuu ni kuondolewa vikwazo haramu na vya kidhalimu Jamhuri ya Kiislamu.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha mwito wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili baina yake na Japan katika nyuga tofauti.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Japan, Hayashi Yoshimasa amesema Tokyo inaunga mkono mazungumzo hayo ya Vienna, na kuondolewa Iran vikwazo ilivyowekewa na Marekani baada ya kujiondoa kwenye mapatano hayo ya dunia 2018.

Mazungumzo ya Vienna

Ametoa mwito kwa washiriki wa mazungumzo ya Vienna kukumbatia fursa iliyopo kwa kufanya juu chini kuhakikisha kuwa makubaliano ya mwisho yanafikiwa.

Kadhalika wanadiplomasia hao wa ngazi za juu wa Iran na Japan mbali na kusisitiza haja ya kuboreshwa uhusiano wa pande mbili, lakini wamegusia pia masuala ya kieneo na kimataifa yenye maslahi ya pamoja kwa Tehran na Tokyo.

 

Tags