Feb 10, 2022 03:37 UTC
  • Raisi: Kuendelezwa sera zilizofeli za Trump ndiyo sababu hasa ya kutopiga hatua mazungumzo ya Vienna

Rais Ebrahim Raisi amesema, kuendelezwa sera zilizofeli za serikali iliyopita ya Marekani ndicho kizuizi kikuu kinachokwamisha kupiga hatua za kuridhisha mazungumzo ya Vienna.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida.

Katika mazungumzo hayo, Rais Raisi amekaribisha hamu na shauku iliyoonyeshwa na Japan ya kustawisha na kuimarisha zaidi  kiwango cha uhusiano na mashirikiano ya pande mbili na akasema: Iran na Japan ni nchi mbili zenye tamaduni na historia kubwa zinazotetea suluhu na amani; na kuimarika uhusiano wao ni kwa manufaa ya mataifa yote.

Seyyid Ebrahim Raisi ameeleza kwamba, kung'ang'ania serikali ya Marekani sera zilizofeli za serikali iliyopita ya nchi hiyo ndicho kizuizi kikuu cha kutopigwa hatua ya kuridhisha katika mazungumzo; na akaongeza kuwa, bila kujali suala la mapatano ya nyuklia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuongeza kiwango cha uhusiano na mashirikiano na nchi zingine ikiwemo Japan kwa manufaa ya pande mbili.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja uingiliaji wa maajinabia kuwa ndio sababu kuu ya kukosekana amani katika eneo; na sambamba na kutilia mkazo kutatuliwa mgogoro wa Yemen kupitia mazungumzo baina ya Wayemen wenyewe, amebainisha kuwa: hivi sasa kuna udharura wa kuuondoa mzingiro wa kidhalimu dhidi ya Yemen ili kuzuia jinai za kutisha za vikosi vya muungano vamizi, za mauaji ya halaiki ya watu wasio na ulinzi wa nchi hiyo.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida ametoa pongezi kwa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na akasema: "nilipokuwa waziri wa mambo ya nje na wakati ninaongoza kundi la urafiki baina ya Iran na Japan nilifanya safari mara kadhaa mjini Tehran; na leo nikiwa na wadhifa wa uwaziri mkuu, kutokana na utambuzi nilionao kuhusu fursa na uwezo wa nchi mbili nimedhamiria kustawisha kiwango cha uhusiano na kuzitumia fursa za ushirikiano wa pamoja kati ya nchi mbili".../

Tags