Feb 25, 2022 06:56 UTC
  • Serikali ya Iran: Vita si suluhisho la mgogoro wowote ule

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vita si suluhisho la tatizo lolote lile. Amesema hayo ikiwa ni kutangaza msimamo wa serikali ya Iran kuhusu vita baina ya Russia na Ukraine huko mashariki mwa Ulaya.

Shirika la habari la ISNA limemnukuu Ali Bahadori-Jahromi akisema hayo kwenye mtandao wa kijamii ya Twitter ambapo ameongeza kuwa: "Vita si utatuzi na kujipendekeza kwa Marekani pia hakuna faida yoyote."

Wakati huo huo Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Russia na kusema kuwa, kitendo cha shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO la kukunjua makucha yake mashariki mwa Ulaya na kwenye mipaka ya Russia ndiko kunakosababisha matatizo.

Wanajeshi wa Ukraine

 

Rais wa Iran amesema, hatua ya jeshi la nchi za Magharibi NATO ya kueneza nguvu zake ni tishio kubwa kwa utulivu na usalama wa nchi huru katika maeneo tofauti duniani.

Jumatano asubuhi, Rais Vladimir Putin wa Russia alitangaza kuanza opereseheni maalumu dhidi ya Ukraine na kusema kuwa, operesheni hiyo inafanyika ili kuzuia kutokea vita vikubwa vya dunia na kuifanya Ukraine isiwe tishio la kijeshi kwa Russia. Alisema, lengo si kuangamiza jeshi la Ukraine wala kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Kiujumla inachopinga Russia ni hatua ya nchi za Magharibi ya kutanua nguvu zao za kijeshi kwenye mipaka ya Russia. Rais Vladimir Putin amesema, kamwe hatoruhusu usalama wa kitaifa wa Russia uchezewe.

Nchi za Magharibi zinadai kuwa Russia imeamua kuikalia kwa mabavu Ukraine na zimeshidisha mno mashinikizo yao ya kidiplomasia na kiuchumi dhidi ya Moscow.

Tags