Mar 11, 2022 08:13 UTC
  • Iran yapinga tuhuma zisizo na msingi za Arab League

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekadhibisha madai yaliyotolewa dhidi ya taifa hili katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Saeed Khatibzadeh amekanusha vikali tuhuma hizo za mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Arab League kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiarabu.

Ameeleza bayana kuwa, Iran imesikitishwa mno na muendelezo huo wa Waarabu wa kuibua madai yasiyo na msingi wowote dhidi ya taifa hili kwa lengo la kulipaka matope.

Khatibzadeh amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inapinga vikali madai hayo ya kukaririwa na yasiyo na msingi yaliyotolewa na nchi ambazo zina historia ndefu ya kuchochea vita na mapigano katika eneo la Asia Magharibi.

Arab League

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amesisitiza kuwa, Tehran inaziasa nchi hizo kutumia njia za mazungumzo na diplomasia kutafutia ufumbuzi suitofahamu zilizopo kati yao na Jamhuri ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa, madai hayo ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu dhidi ya Iran hayana matokeo mengine isipokuwa kuweka vizingiti katika jitihada za kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo na Jamhuri ya Kiislamu.

Tags