Mar 20, 2022 07:43 UTC
  • Makubaliano ya Vienna hayataifanya Iran iache kufuatilia faili la mauaji ya Soleimani

Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Idara ya Mahakama ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haitaacha kuwafuatilia wahusika wa mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), kwa sababu ya makubaliano ya mazungumzo ya Vienna.

Kazem Gharib Abadi amesema kamati ya pamoja ya uchunguzi ya Iran na Iraq imekuwa ikikutana mara kwa mara na kutoa taarifa za pamoja kuhusu faili hilo la mauaji ya kigaidi ya Shahidi Soleimani, na hadi sasa Tehran imepokea nyaraka zenye kurasa zaidi ya 1000 za kadhia hiyo kutoka Baghdad.

Ameeleza kuwa: Kutokana na idadi kubwa ya wahanga wa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Iran uliosababishwa bila shaka na mienendo ya Wamagharibi wakiongozwa na Marekani; hususan ugaidi na vikwazo-lazima kila siku tutume madazeni ya malalamiko kwa taasisi za haki za binadamu duniani.

Jenerali Soleimani aliuawa kidhulma uraiani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, tena akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq mnamo Januari 3 mwaka 2020.

Aliuawa shahidi kwa amri ya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump akiwa pamoja na wanamuqawama wenzake tisa akiwemo Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu wa Mkuu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al Hashdu al Shaabi.

Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Idara ya Mahakama ya Iran amekumbusha kuwa, Wairani zaidi ya 17,000 wameuawa na makundi mbalimbali ya kigaidi likiwemo la MKO, baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Tags