Mar 30, 2022 11:48 UTC
  • Saeed Khatibzadeh
    Saeed Khatibzadeh

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema kuwa bara la Afrika lina nafasi ya juu kabisa katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Saeed Khatibzadeh ambaye alikuwa akizungumzia safari yake ya karibuni nchini Senegal, amesema kuwa, mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Dakar na viongozi wa jumuiya za kijamii za nchi hiyo ambayo ni lango la eneo la Magharibi mwa Afrika, vilevile ametembelea kisiwa cha Gorée kinachokumbusha ukatili usio na mfano wa kipindi cha ukoloni wa nchi za Magharibi barani Afrika. 

Wakoloni wazungu walikuwa wakisafirisha watumwa kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika hadi kwenye kisiwa cha Gorée huko Senegal, na kisha wanahamisha eneo hilo la kuwapeleka kuwauza Amerika na nchi za Magharibi kwa kutumia meli.

Kisiwa cha Gorée, karibu na pwani ya Dakar, Senegal, kinaaminika kuwa kituo kikuu cha maelfu ya kwa maelfu ya watumwa waliokuwa wanasafirishwa kikatili kwenda Amerika katika karne ya 16 mpaka 19.

Kisiwa cha Goree, Senegal

Kwenye kisiwa hiki kunapatikana nyumba ya makumbusho ya watumwa ambayo ilikuwa ikihifadhi kati ya watumwa 150 mpaka 200 kwa wakati mmoja wakisubiri kusafirishwa na wazungu na kuuzwa kwenye mataifa ya Magharibi.

Nchi ya Senegal yenye eneo lenye ukubwa wa kilomita mraba 196,190, iko Magharibi kabisa mwa Afrika na inashirikiana mpaka na Mauritania, Mali, Guinea-Conakry, Guinea-Bissau na Gambia, na upande wa Magharibi inapakana na Bahari ya Atlantiki.

Tags