Apr 03, 2022 11:28 UTC
  • Amir Abdollahian azungumza kwa simu na Guterres: Mapatano yanakaribia katika mazungumzo ya Vienna

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa mapendekezo ya Iran katika mazungumzo ya Vienna yametumwa upande wa Marekani mwakilishi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo hayo; na sasa mpira upo mbele ya Marekani.

Hossein Amir-Abdollahian amezungumza kwa simu na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu matukio ya karibuni kuhusu mazungumzo ya kuondoa vikwazo dhidi ya Iran huko Vienna na kuongeza kuwa: pande shiriki katika mazungumzo hayo zinakaribia kufikia makubaliano na masuala yaliyosalia tayari yamefikishwa kwa Marekani kupita mkuu wa timu ya mazungumzo wa Umoja wa Ulaya. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameeleza kufurahishwa na kufikiwa usitishaji vita huko Yemen na amepongeza jitihada za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika uwanja huo na kueleza kuwa, wakati umefika sasa wa kuchukuliwa hatua kuu na muhimu za kurejesha amani na uthabiti huko Yemen na hasa kuondoa kikamilifu vikwazo vya kidhalimu walivyowekewa wananchi Waislamu wa nchi hiyo.  

Vita vya Saudia huko Yemen 

Amir Abdollahian amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuunga mkono juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen ili kuhitimisha vita nchini humo. Aidha ameeleza matarajio yake kuwa, mzingiro waliowekewa wananchi wa Yemen pia unapasa kuondolewa kikamilifu sambamba na kuheshimiwa usitishaji vita nchini humo. Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amekaribisha ziara ya Hans Grandberg, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Yemen na ajenda ya kazi ya Baraza la Usalama kwa ajili ya kuwasilisha taarifa mbili tofauti kuhusu Yemen na kuongeza kuwa: Iran inaunga mkono kutolewa taarifa hizo na Baraza la Usalama zinazounga mkono usitishaji vita Yemen. Amesema, taarifa nyingine zinatolewa kwa kufuata misimamo ya upande mmoja na bila ya kutilia maanani mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen na zinazoishutumu Serikali ya Ukokovu wa Kitaifa ya Yemen hazina maana yoyote. 

Katika mazungumzo hayo ya simu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyataja mazungumzo ya Vienna kuwa ni yenye umuhimu mkubwa na amesema, anataraji kuwa pande husika katika mazungumzo hayo zitafika makubaliano hivi karibuni. Guterres aidha ametoa mkono wa kheri kwa kuwadia mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuongeza kuwa, Umoja wa Mataifa utaiweka katika ajenda yake ya utendaji Mpango kwa jina la "Ramadan Solidarity Initiative"  unaolenga kurejesha amani na kuwezesha hatua za kibidamu huko Yemen.  

Tags