Apr 23, 2022 02:35 UTC
  • Waafghani wote walioko Iran wamepokea chanjo ya bure ya COVID-19

Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema raia wote wa Afghanistan wanaoshi kama wakimbizi hapa nchini wamepigwa chanjo ya kupambana na ugonjwa wa COVID-19 bila malipo.

Bahram Einollahi, Waziri wa Afya wa Iran alisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa: Mbali na Waafghani wote wanaoishi nchini kunufaikia na Mpango wa Kitaifa wa Chanjo Dhidi ya COVID-19, lakini pia aghalabu yao walioakumbwa na maradhi hayo walilazwa na kutibiwa bila malipo katika hospitali na vituo mbalimbali vya  afya hapa nchini.

Einollahi ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haijawawekea vizingiti vyovyote mamilioni ya wakimbizi wa Afghanistan wanaoishi hapa nchini, haswa ikija katika masuala ya matibabu na huduma za afya.

Wakati huohuo, Bahram Einollahi, Waziri wa Afya wa Iran amelaani vikali mauaji ya kikatili ya Waislamu katika shambulio la kigaidi la Alkhamisi dhidi ya msikiti wa Waislamu wa Kishia huko Mazar-Sharif katika mkoa wa Balkh nchini Afghanistan.

Amesema inasikitisha matukio hayo ya kusikitisha dhidi ya Waislamu hususan wa Kishia huko Afghanistan yanafanyika katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuwapelekea misaada ya kibinadamu hususan matibabu wananchi wa taifa dugu na rafiki la Afghanistan.

Raia wa Afghanistan wakisubiri chanjo ya Corona nchini Iran

Katika hatua nyingine, vituo vya kiafya katika mkoa wa Khorasan Kusini, mashariki mwa Iran vimejiandaa kwa ajili ya kuwapa chanjo ya MMR maelfu ya raia wa kigeni mkoani hapo.

Majid Shayesteh, Naibu Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba cha Birjand aliliambia shirika la habari la IRNA jana Ijumaa kuwa, mkoa wa Khorasan Kusini umeanzisha kampeni ya kutoa chanjo ya MMR ya kuzuia ukambi, matumbwitumbwi (mumps) na rubella kwa raia wa kigeni wapatao 6,800 wanaoishi mkoani hapo.

 

Tags