May 05, 2022 07:19 UTC
  • Majid Takht-e-Ravanchi
    Majid Takht-e-Ravanchi

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amevitaja vikwazo na hujuma dhidi ya Uislamu (Islamophobia) katika nchi za Magharibi kuwa ni kinyume na kanuni, sheria za kimataifa, sheria ya kibinadamu na Hati ya Umoja wa Mataifa, na ametoa wito kwa idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya umoja huo kuendeleza juhudi za kukabiliana na athari mbaya za vikwazo vya upande mmoja kwa nchi zilizoathiriwa na vikwazo.

Majid Takht-e-Ravanchi ambaye alikuwa akihutubia Kamati ya Mawasiliano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amelaani vikwazo hivyo haramu vya upande mmoja na kusema kuwa vinazidisha matatizo ya kiuchumi, kibiashara na kifedha kwa nchi zilizolengwa, kudhoofisha ustawi wa uchumi, na kuzuia upatikanaji wa vifaa tiba na malighafi kutokana na kuzuia upatikanaji wa fedha za kigeni.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Kwa bahati mbaya, baadhi ya nchi zinaendelea kutumia ukiritimba wa teknolojia zao za kisasa za mawasiliano ili kupotosha na kupindua ukweli wa mambo katika nchi nyingine hususan nchi zinazoendelea na hivyo kuchafua sura na maslahi ya nchi hizo; hivyo jamii ya kimataifa inapaswa kushughulikia hali hiyo haraka iwezekanavyo. 

Majid Takht-e-Ravanchi

Akizungumzia hali inayoongezeka ya hujuma na chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi, Takht-e Ravanchi amesema: "Kujenga mazingira ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika sehemu mbalimbali za dunia kunakochochewa na  vyombo vya habari vinavyopinga Uislamu na matamshi ya uchochezi na chuki ya baadhi ya wanasiasa katika nchi za Magharibi vinatia wasiwasi mkubwa."

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: "Umefika wakati kwa jamii ya kimataifa kulaani jambo hilo na kuchukua hatua zinazohitajika ili kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na ukiukaji wa haki za kimsingi za Waislamu."

Tags