May 15, 2022 11:01 UTC
  • Iran yalaani ukiukwaji mpya wa haki za binadamu uliogundulika Marekani

Kazem Gharibabadi, Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa taarifa baada ya uchunguzi kubaini vifo vya zaidi ya watoto 500 wa jamii za asili za Marekani katika shule za bweni za kanisa, zilizofadhiliwa na serikali na kusema: "Pamoja na kuwepo ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu huko Marekani nchi hiyo inajipa jukumu la kuwapa wengine nasaha kuhusu haki za binadamu."

Gharibabadi ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Watoto wa jamii asili za Marekani walitengwa na familia zao, walizuiwa kuzungumza lugha ya asili, waliteswa, walinajisiwa na kubakwa kisha wakatuppwa katika makaburi ya umati kisha Marekani inajipa idhini ya kuwanasihi wengine kuhusu haki za binadamu."

Kuwatenganisha watoto wa jamii za asili za Marekani na familia zao, na hali kadhalika kuwateganisha na lugha na utamaduni wao sambamba na kuwapa elimu ya lazima na kisha kuwaua kwa umati baadhi yao ni ukurasa mchafu katika historia ya Marekani ambapo wakoloni wazungu waliokuwa wamehamia nchini humo walitekeleza mkakati maalumu wa kuwaangamiza kwa makusudi wakaazi asili wa Amerika Kaskazini. Jinai iliyotendeka wakati huo ilikuwa kubwa kiasi kwamba hata serikali ya sasa ya Marekani haina budi ila kukiri kuhusu ukatili na ukiukaji huo mkubwa wa haki za binadamu.

Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani Deb Haaland hivi karibuni alitangaza kuwa uchunguzi umebaini kuwepo makaburi mengi yasiyo na alama katika shule za bweni ambapo watoto Wamarekani asili walilazimishwa kwenda. Amesema kuna maeneo 52 yaliyodungulidika yenye makaburi hayo ya umati na kuongeza kuwa, watoto katika shule hizo za bweni waliteswa, kubakwa na kudhulumiwa kinafsi na hayo yote yako kwenye rekodi. Aidha amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwepo makaburi ya umati ya zaidi ya watoto 500 katika shule hizo za bweni. Akizungumza katika mkutano wa wanahabari siku ya Jumatano, Haaland alielezea jinsi enzi ya shule ya bweni iliendeleza umaskini, matatizo ya afya ya akili, matumizi mabaya ya dawa za kulevya na vifo vya mapema katika jamii za wakazi asili wa Marekani.

Kazem Gharibabadi, Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Pamoja na kuwa tawala mbali mbali za Marekani zimekuwa zikitoa nara za kudai kuunga mkono haki za binadamu na uhuru wa mtu binafsi na kijamii nchini humo lakini kivitendo tawala za nchi hiyo zimekuwa zikitekeleza vitendo vya utumiaji mabavu, vya kibaguzi na vyenye kukiuka haki za binadmau dhidi ya Waamerika asili, jamii za waliowachache hasa Waislamu na watu wenye asili ya Afrika. Hali kadhalika katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Marekani imekuwa ikiwatendea unyama wakimbizi ikiwa ni pamoja na kuwatenganisha  watoto na wazazi wao. Aidha hali ya wafungwa katika magereza ya Marekani ni mbaya sana ambapo aghalabu ya wafungwa ni Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao wanakumbwa na masaibu mengi sana katika nchi hiyo. Hiyo ni mifano michache tu ya ukiukwaji mkubwa na wa wazi wa haki za binadamu unaofanywa nchini Marekani. 

Hali kadhalika baada ya kuibuka virusi vya COVID-19, waliowachache nchini Marekani walikumbwa na matatizo mengi, Jamii za Wamarekani wenye asili ya Afrika, Walatino na Wamerika Asili walidhuriwa zaidi na janga la COVID-19 ikilinganishwa na wazungu. Jambo hilo linaashiria ubaguzi mkubwa wa rangi ulioko Marekani katika sekta za afya, makazi, maji safi na ajira. Aidha matajiri, ambao wengi ni wazungu wamezidi kutajirika huku raia wengine wa nchi hiyo wakizidi kuwa masikini.

Marekani ambayo ni kinara wa nchi za Magharibi imekuwa ikidai kuwa ni mtetezi wa uhuru na haki za binadamu na kila mwaka hutoa ripoti ndefu ya kimataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika nchi zingine duniani hasa nchi hasimu na shindani kwa malengo ya kipropaganda. Hii ni katika hali ambayo, Marekani yenyewe ni mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani.

Andranik Migranyan mtaalamu wa masuala ya kimataifa nchini Russia anasema:" Marekani inakiuka haki za binadamu kuliko nchi nyingi yoyote duniani." Swali ambalo wengi wanaliuliza ni kuwa je, ni kitu gani kinaipelekea Marekani ijione kuwa inastahiki kutoa kauli kuhusu haki za binadamu katika nchi zingine huku ikipuuza yanayojiri ndnai ya ardhi yake"

Mauaji ya George Floyd  ni mfano mdogo tu wa namna haki za Wamarekani wenye asili ya Afrika zinavyokiukwa mikononi mwa polisi na taasisi rasmi nchini Marekani

Asasi za kimataifa za haki za binadamu kama vile Baraza la Usalama la Haki za Binadamu zimekuwa zikitoa taarifa za mara kwa mara kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu unaotokelezwa rasmi na taasisi za nchi hiyo hasa ubaguzi dhidi ya Waamerika Asili na watu wenye asili ya Afrika. Kufichuliwa mauaji ya umati ya watoto Waamerika Asili katika shule za bweni za kanisa zilizokuwa zikifadhiliwa na serikali ni kashfa ya hivi punde zaidi ya ukiukaji wa haki za binadamu huko Marekani. Kashfa hiyo imejiri katika nchi ambayo imekuwa ikidai kuwa ni kinara wa kulinda haki za binadamu duniani. Serikali yenye kiburi ya Marekani imekaidi matakwa ya taasisi za kutetea haki za binadamu ambazo zimeitaka izingatie haki za Waamerika asili na watu wa kaumu zingine zisizo za wazungu, hasa Wamarekani wenye asili ya Afrika na Waislamu.

 

Tags