May 17, 2022 12:31 UTC
  • Iran: Mazungumzo ya kuondolewa vikwazo yanaendelea ili kutatua masuala yaliyobaki

Abbas Golroo, mjumbe wa kamati ya usalama wa taifa na sera za nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema, kwa mujibu wa mashauriano ya karibuni yaliyofanywa na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, mazungumzo ya kuondolewa vikwazo yanaendelea ili kutatua masuala yaliyobaki.

Awali, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Saeed Khatibzadeh alieleza kwamba, mazungumzo ya maana yalifanyika wakati wa safari ya siku kadhaa zilizopita ya mjumbe mwandamizi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo Enrique Mora, ambapo mwanadiplomasia huyo wa EU na Ali Baqeri, mjumbe mwandamizi wa Iran katika mazungumzo, walifanya mazungumzo na mashauriano ya duru kadhaa.

Siku ya Jumanne iliyopita, Mora alikuja hapa mjini Tehran na kufanya mazungumzo ya saa kadhaa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ai Baqeri.

Iran na Umoja wa Ulaya zinaamini kuwa vikao hivyo vilivyofanyika baina ya pande mbili vimetoa fursa mpya kwa pande hizo kujikita katika kufanya ubunifu wa kutatua masuala yaliyosalia katika mazungumzo ya Vienna.

Abbas Golroo

Wakati huohuo Abbas Golroo, mjumbe wa kamati ya usalama wa taifa na sera za nje ya Bunge la Iran amesema, majlisi hiyo ya ushauri ya Kiislamu inaunga mkono mazungumzo; na Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu pia inayaangalia kwa mtazamo chanya mazungumzo hayo ili yaweze kupatikana matunda ya majadiliano yaliyodumu kwa muda wa miezi kadhaa, hata hivyo shughuli za nchi hazitacheleweshwa na matokeo ya mazungumzo hayo.

Serikali ya Marekani inayoongozwa na Joe Biden, ambayo imekuwa ikidai kuwa inafuata muelekeo wa kidiplomasia katika kuamiliana na Iran na kufanya jitihada za kuhakikisha inarudi kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, hadi sasa haijachukua hatua yoyote ya maana kuonyesha kuwa ina njema juu ya suala hilo.../