May 19, 2022 07:12 UTC
  • Iran: Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeifedhehesha kwa mara nyingine Marekani

Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatua ya ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa ya kukiri kuwa, vikwazo ilivyowekewa Iran si halali na ni kinyume maadili ya kibinadamu, ni fedheha nyingine iliyoikumba Marekani.

Ali Bahadori Jahromi amesema hayo akiashiria ziara ya Bi Alena Douhan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iran na kuandika: Mwishoni mwa ziara yake hapa Iran, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa amethibitisha kuwa, hatua za upande mmoja zilizochukuliwa na Marekani dhidi ya Tehran si halali na ni kinyume na maadili ya kibinadamu na sheria zote za kimataifa.

Bahadori Jahromi aidha amesema, Marekani inapaswa kuondoa mara moja vikwazo vyote ilivyoiwekea Iran.

Alena Douhan akizungumza na mwaandishi wa habari mjini Tehran

 

Jana Jumatano, Bi Alena Douhan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iran aliwaambia waandishi wa habari hapa Tehran kuwa, vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinavunja haki za binadamu na akaitaka Marekani iondoe vikwazo hivyo ilivyoiwekea Tehran bila ya sababu yoyote.

Vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran vinajumuisha pia mahitaji ya kimsingi ya wananchi mpaka madawa na vifaa vya matibabu na vimewasababishia matatizo mengi wananchi wa kawaida wa Iran hasa wale wenye magonjwa maalumu na sugu.

Kabla ya hapo pia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alkuwa amethibitsha kwamba vikwazo vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran vimewaletea matatizo mengi wananchi wa kawaida na pia vinakwamisha huduma za kibinadamu nchini Iran.