May 19, 2022 12:49 UTC
  • Khatibzadeh: Mapinduzi ya Kiislamu yameutambulisha kwa ulimwengu utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu amesema, Mapinduzi ya Kiislamu yameutambulisha duniani utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi.

Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo leo alipohutubia kongamano la ufanyaji tablighi ya dini kimataifa lililoendelea kwa siku ya pili katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Jaamiatul-Must'afa mjini Mashhad kwenye mkoa wa Khorasane-Razavi kaskazini mashariki ya nchi.

Jaamiatul-Must'afa al Aalamiyyah ni taasisi ya elimu ya kimataifa ya hapa nchini Iran yenye muundo wa chuo cha kidini, Hawza ambayo lengo la kuasisiwa kwake ni kueneza elimu za Kiislamu na za Kijamii kwa kufuata mfumo wa kimafunzo, kiutafiti na kimalezi na inajumuisha idadi kubwa wanafunzi kutoka kila pembe ya dunia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, katika hotuba aliyotoa kwenye kongamano hilo lililoanza jana na kumalizika leo, Khatibzadeh amesema, badala ya Ukomunisti na Ubepari, Mapinduzi ya Kiislamu yaliitambulisha kwa ulimwengu njia ya tatu ya Mfumo wa Utawala wa Kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi; na matunda yake leo hii inapasa yawe ni ya kuurejesha tena Ustaarabu Mkubwa wa Kiislamu; na katika kufikia lengo hilo wafanyatablighi ya dini wana nafasi na mchango muhimu sana.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, dunia na misamiati ya mawasilianao ya kimataifa na kidiplomasia vimo kwenye hali ya kubadilika; na tunachoshuhudia leo hii ni mmiminiko wa jumbe mbalimbali zinazotumwa kwa kutumia nyenzo na mbinu za kisasa. Kwa hiyo katika hali na mazingira haya inatupasa tujifahamu tuko wapi na kuingia kwenye awamu mpya kwa kuzingatia misimiati hiyo.

Khatibzadeh amesisitiza pia kuwa, moja ya kazi muhimu zaidii katika uga wa elimu, utafiti na tablighi ya dini na Qur'ani kimataifa inafanywa na Jaamiatul-Must'afa.../

 

 

Tags