May 20, 2022 03:08 UTC
  • Iran: Ikiwa Marekani itachukua hatua kimantiki, mwafaka utaweza kupatikana

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa ikiwa Marekani itachukua hatua kimantiki, mwafaka utaweza kupatikana.

Serikali ya Marekani inayoongozwa na Joe Biden, ambayo imekuwa ikidai kuwa inafuata muelekeo wa kidiplomasia katika kuamiliana na Iran na kufanya jitihada za kuhakikisha inarudi kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, hadi sasa haijachukua hatua yoyote ya maana kuonyesha kuwa ina nia njema juu ya suala hilo.

Takriban nchi zote zinazoshiriki katika mazungumzo ya Vienna zinataka mazungumzo hayo ya nyuklia yakamilishwe haraka iwezekanavyo, lakini kufikiwa mwafaka na makubaliano rasmi kunasubiri maamuzi ya kisiasa yanayopasa kuchukuliwa na Marekani kuhusu maudhui kadhaa kuu na muhimu zilizosalia.

Katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu hapo jana na mwenzake wa Russia Sergey Lavrov kuhusiana na mazungumzo ya Vienna na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, ikiwa Marekani itachukua hatua kimantiki, mwafaka utaweza kupatikana.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongezea kwa kusema: "Tunataka pande zote husika zifikirie hatua ya kuchukuliwa kuhusiana na mazungumzo."

Amir-Abdollahian amebainisha pia kwamba, Tehran ina nia ya dhati ya kufikia mwafaka mzuri, madhubuti na wa kudumu; na bila ya shaka kwa kuzingatiwa mistari yake myekundu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vilevile amesema, msimamo chanya wa Russia katika kuunga mkono makubaliano yanayokubaliwa na Iran ni wa kupongezwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza katika mazungumzo hayo kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za kuhakikisha mwafaka unafikiwa katika mazungumzo ya Vienna.

Lavrov ameongeza kuwa, Moscow inafanya jitihada ili kuweza kupatikana mwafaka wa kiuadilifu utakaodhamini matakwa na maslahi ya Iran.../