May 21, 2022 07:31 UTC
  • Iran ina azma ya kufikia mapatano imara katika mazungumzo ya Vienna

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina azma ya kufikia mapatano mazuri, imara na ya kudumu na nchi za Magharibi katika mazungumzo ya Vienna.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo Ijumaa jioni katika majadiliano ya simu na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya kuhusu mazungumzo ya Vienna yanayofanyika kwa ajili ya kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran.

Amir-Abdollahian ameashiria kuendelea mashauriano kuhusu Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema,  hakuna shaka kuwa serikali ya Iran inataka kufikia mapatano mazuri, imara na ya kudumu.

Akiashiria safari ya hivi karibuni mjini Tehran ya Enrique Mora, Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Ulaya, Amir-Abdollahian amesema mapendekezo kadhaa yalijadiliwa katika safari hiyo na kuongeza kuwa Iran ina azma ya kufikia mapatano mazuri. Akiashiria mgogoro wa Ukraine, amesema Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikisisitiza kuwa inapinga vita vyovyote vikiwemo vinavyoendelea Ukraine.

Mazungumzo ya nyuklia ya Vienna

Aidha amesema Iran iko tayari kupatanisha mgogoro wa Ukraine huku akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono amani na usalama.

Kwa upande wake Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya ameashiria mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna na kusema: "Tumechukua mkondo mpya wa kuendeleza mazungumzo ili kupata suluhisho?

Borrelll ameendelea kusema kuwa, Umoja wa Ulaya una azma ya kuendeleza jitihada za mawasiliano yaliyopo baina ya Tehran na Washington ili kukurubisha maoni ya pande mbili. Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya ameelezea matumaini yake kuwa jitihada hizo zitazaa matunda.

Hali kadhalika Borrell ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa jitihada zake za kuutatua mgogoro wa Ukraine na kusema jitihada za Iran kualika pande husika katika mazungumzo ni ishara ya nia njema ya Tehran.

Amesema la kusikitisha ni kuwa pande mbili zinatuhumiana kuhusu kukosekana nia njema ya mazungumzo na kwa msingi huo, katika hali kama hiyo ni vigumu kufikia mapatano.