May 23, 2022 03:45 UTC
  • Iran ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazotengeneza na kurusha satelaiti katika anga za mbali

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Issa Zarepour amesema, Iran ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazotengeneza na kurusha satelaiti katika anga za mbali na kusisitiza kuwa sekta hiyo inailetea Iran nguvu na teknolojia mpya.

Zarehpour amesema: Iran imepata maarifa na teknolojia ya hali ya juu zaidi katika uga wa anga za mbali katika kilele cha vikwazo na matatizo, kwa kadiri kwamba imefanikiwa kutengeneza satelaiti na makombora ya kurushia satelaiti ambayo yanazifikisha satelaiti hizo katika maeneo yaliyokusudiwa angani kwa usahihi na umakinifu mkubwa. Huku akibainisha kuwa nchi kama Uingereza kwa hivi sasa bado zinaitegemea Russia kuzirushia satelaiti, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran amesema ni fahari kubwa kwamba hii leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajivunia kuwa moja ya nchi zilizo na uwezo mkubwa na teknolojia ya kisasa kabisa katika uwanja huo. Katika kilele cha vikwazo na matatizo, Iran imepata maarifa na teknolojia ya hali ya juu zaidi katika uwanja wa anga za juu ambayo inaiwezesha kujitengenezea satelaiti na makombora ya kurushia satelaiti na kuziweka kwa usahihi na ustadi mkubwa katika maeneo yanayolengwa angani.

Katika miongo minne iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua kubwa za maendeleo katika uga wa kujipatia teknolojia ya makombora yanayofika katika anga za mbali. Hata kama maadui wamejaribu kukwamisha maendeleo ya kiuchumi na kisayansi ya Iran, ikiwemo sekta ya anga za mbali, kupitia vikwazo mbalimbali, lakini licha ya vikwazo na mashinikizo hayo yote, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa pakubwa kupata teknolojia mbalimbali za masuala ya anga za mbali, jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa kuwa ni maendeleo makubwa kwa Iran ya Kiislamu.

Satelaiti ya Iran ikitayarishwa kurushwa angani

Iran hivi sasa ni miongoni mwa nchi 10 za dunia zenye uwezo mkubwa katika anga za juu, mafanikio ambayo yamepatikana kutokana na juhudi za zaidi ya miongo 4 za wataalamu wa humu nchini, na kwa hivyo Iran ina nafasi muhimu katika sekta hii kati ya nchi chache zilizo na teknolojia hiyo. Hivi sasa, ujenzi wa vituo vya kurushia satelaiti uko mikononi mwa nchi 6 tu, na Iran iko kwenye nafasi inayofuata katika uwanja huo wa kustawisha vituo vya anga za mbali.

Sekta ya anga za juu ni moja ya tasnia zinazohitajia teknolojia ya hali ya juu. Licha ya vikwazo vyote hivyo, lakini kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kupata na kudhibiti mzunguko kamili wa teknolojia ya anga za juu. Kubuni na kutengeneza makombora ya kurushia satelaiti na hatua muhimu katika kutengeneza satelaiti zinazoundwa ndani ya nchi, kuzirusha angani, kupokea data na hatimaye kutumia data zilizopokelewa huunda mzunguko kamili wa teknolojia hii. Tofauti kubwa iliyopo kati ya mpango wa anga za juu wa Iran na nchi nyingine za eneo la Asia Magharibi ni kwamba Iran inategemea uwezo wake wa ndani na kunufaika na teknolojia yake ya asili bila kuwategemea wageni.

Wakati huo huo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Iran imezingatia na kupiga hatua kubwa katika uwanja wa kutengeneza makombora ya kurushia angani satelaiti ambapo imekuwa ikitenegeneza makombora ya aina hiyo sambamba na kutengeneza satalaiti zenyewe. Wataalamu wa Iran hivi sasa wamefikia na kudhibiti mzunguko kamili wa teknolojia ya anga za juu, yaani ujuzi wa kujenga kituo cha kurushia satalaiti, makombora ya anga za mbali, kituo cha kupokea na kudhibiti satelaiti na kituo cha data zinazotumwa na satelaiti.

Mojawapo ya mafanikio muhimu ya hivi karibuni ya Iran katika anga za mbali na ambayo yalizinduliwa mnamo Machi 2022, ni satelaiti ya Noor 2. Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la IRGC, anasema: “Hatuna budi ila kufika katika anga za mbali na katika siku zijazo tutazindua satelaiti kadhaa katika mfululizo wa satelaiti za Noor.” Ali Bahadori Jahromi, Msemaji wa Serikali ya Iran, amesema: Kuiona dunia kutoka angani kupitia satelaiti za Iran ni mafanikio makubwa ya kimkakati."

Satelaiti ya Noor 2 ikitumwa katika anga za mbali

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu huku akibainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi ya kwanza ya Kiislamu kurusha satelaiti angani amesema: Leo tumeweza  kumshinda adui na kufanikiwa kupata teknolojia hii ngumu na elimu ya kisasa, na hivyo kuibadilisha kuwa bidhaa yenye umihimu na mafanikio makubwa. Satelaiti za Noor 1 na Noor 2 ni satelaiti za kwanza za kijeshi nchini Iran kuwahi kuwekwa katika mzunguko wa sayari katika anga za mbali. Kwa jumla, ni nchi 30 tu ulimwenguni ndizo zina satelaiti kama hizo katika anga za mbali.

Tags