May 23, 2022 03:52 UTC
  • Askari wa IRGC Mlinzi wa Haram auawa shahidi katika hujuma ya kigaidi

Idara ya Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imetangaza kuwa mmoja wa askari wake ambaye ni Mlinzi wa Haram ameuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi mjini Tehran Jumapili jioni.

Kwa mujibu wa taarifa ya IRGC, askari mwenye kuheshimika mlinzi wa Haram Kanali Hassan Sayyad Khodaei ameuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi ya wapinga Mapinduzi ya Kiislamu na maajenti wa madola ya kiistikbari duniani.

Taarifa ya IRGC imeongeza kuwa: "Leo (Jumapili) katika moja ya vichochoro vinavyoelekea Barabara ya Mujahidina Islam mashariki mwa Tehran, mlinzi wa Haram, Kanali wa IRGC Sayyad Khodaei amelengwa katika jinai ya kigaidi ya walio dhidi ya Mapinduzi ambao ni maajenti wanaofungamana na uistikbari wa kimataifa."

Shahidi Hassan Sayyad Khodaei akiwa ndani ya gari lake baada ya kupigwa risasi

IRGC imetuma salamu za pongezi sambamba na rambirambi kwa familia ya Kanali Khodaei na kusema: "Hatua za lazima zimechukuliwa kwa ajili ya kutambua na kukamata mhusika au wahusika wa jinai hiyo."

Shahidi Sayyad Khodaei ameuawa shahidi kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya gari lake mbele ya nyumba yake.

Kufuatia jinai hiyo, Jaji wa Mahakama ya Uadilifu Tehran, Ali Alqasi amemuamuru Mwendesha Mashtaka wa Tehran achukue hatua za haraka za kuwakamata waliohusika na jinai hiyo.

Wakati huo huo, tovuti ya Nour News, iliyo karibu na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, imechapisha taarifa katika ukruasa wake wa Twitter na kutaja hatua ya mauaji ya Shahidi Khodaei kuwa "ni kuvuka mstari mwekundu jambo ambalo litabadilisha mahesabu mengi." Aidha taarifa hiyo imesema waliopanga mauaji hayo na waliyoyatekeleza watapata adhabu kali.

 

Tags