May 23, 2022 07:20 UTC
  • Iran yajikarabatia kikamilifu ndege za kivita aina ya F-14

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kujikarabatia kikamilifu ndege ya kivita ya Kimarekani F-14 kwa kutegemea wataalamu wa Kikosi cha Anga na mashirika ambayo msingi wake ni elimu nchini na sasa ndege hiyo inaruka angani kama kawaida.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliutaja mwaka mpya wa 1401 Hijria Shamsia ulioanza Machi 21 kuwa ni mwaka wa "uzalishaji, msingi wa elimu na kubuni nafasi za ajira" na hivyo ustawi wa mashirika ambayo msingi wake ni elimu ni moja ya njia bora zaidi za kubuni nafasi mpya za ajira.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Brigedia Jenerali Hamid Vahedi Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ndege hiyo ya kivita ya F-14 ya kikosi hicho sasa imeweza kuruka angani tena baada ya kusimamishwa kwa miaka 18. Amesema ndege hiyo imefanyiwa ukarabati kamili (overhaul) katika Kituo cha Ndge za Kivita cha Shahid Babai mjjini Isfahan.

Brigedia Jenerali Vahedi amesema adui hakudhani hata siku moja kuwa Iran ingeweza kukarabati ndege hizo za F 14 zenye teknolojia ya kipekee na ambazo utunzaji wake ni mgumu sana.

Aidha amesema ukarabati wa ndege ya kwanza  ya F-14 umechukua muda wa miaka mitatu  na kwamba sasa ndege hiyo imeanza kutekeleza oparesheni zake na itakuwa na nafasi ya kuimarisha uwezo wa kivita na kiulinzi nchini.

Ndege ya kivita ya F-14 ikiwa imesheheni silaha

Brigedia Jenerali Vahedi amesema mchakato mzima wa kukarabati ndege hii ya kivita umetumia maelfu ya vipuri  na kuongeza kuwa, ukarabati huu umetekelezwa kwa asilimia 100 na wataalamu Wairani.

Ndege hizo za F-14 zilinunuliwa kutoka Marekani na utawala wa kifalme uliokuwa ukitawala Iran kidikteta na ambao ulikuwa kibaraka wa Marekani.

Hata hivyo kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka wa 1979 Marekani ilikataa kuipa Iran vipuri na ramani za ukarabati wa ndege hiyo.

Mwaka jana pia Iran ilitangaza kuwa imefanikiwa kukarabati kikamilifu ndege nyingine ya kivita ya Kimarekani aina ya F-5 kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi bila msaada wowote wa kigeni.