May 23, 2022 10:45 UTC
  • Iran; mhanga na mlengwa wa kila mara wa ugaidi

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hakikisho kuwa, damu ya Shahidi Hassan Sayyad Khodaei italipiziwa kisasi na akasisitiza kwamba, hakuna shaka mkono wa Uistikbari wa dunia unaonekana katika mauaji hayo.

Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena wamedhihirisha dhati yao chafu na ovu baada ya kumuua shahidi kwa kumpiga risasi tano Kanali Hassan Sayyad Khodaei, Mlinzi wa Haram, katika shambulio la kinyama walilofanya jana Jumapili hapa mjini Tehran.

Akizungumza mapema leo kabla ya kuelekea Oman, Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza: "bila ya shaka katika jinai hii unaonekana mkono wa Uistikbari wa dunia na watu walioshindwa na Walinzi wa Heshima na Haram, ambao kwa kutumia njia hiyo wanataka kuonyesha walivyokatishwa tamaa."

Rais Ebrahim Raisi

Iran ni moja ya nchi waathirika na wahanga wakubwa zaidi wa ugaidi duniani, ambapo hadi sasa watu laki moja na 70 elfu miongoni mwa raia na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameuliwa shahidi katika mashambulio na hujuma za kigaidi.

Kuanzia siku za mwanzoni mwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, sambamba na kuvurugika mahesabu ya nguvu za Uistikbari wa dunia, Iran ilianza kuandamwa na wimbi la chuki na uhasama wa maadui, maajenti na vibaraka wao likiwemo genge la Munafikina la MKO. Katika kipindi cha kuanzia tarehe 31 Machi 1983 hadi Machi 6, 1984, genge hilo la MKO lilikiri kuhusika na mauaji ya watu 4,583 nchini Iran.

Katika miaka ya karibuni, Marekani na utawala wa Kizayuni, kila mara zimekuwa zikitoa misaada na uungaji mkono kwa magaidi ndani ya Iran na katika eneo hili. Utoaji mafunzo kwa wanachama wa makundi ya kigaidi, kuwapatia shehena za silaha zikiwemo nyepsi na nzito pamoja na mitambo ya mawasiliano na kufikisha shehena za vyakula kwa njia ya anga katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la kigaidi la DAESH (ISIS), ni sehemu ndogo tu ya misaada na uungaji mkono wa Washington kwa magaidi ambao wametumiwa na Marekani yenyewe kwa njia tofauti na kwa ajili ya kudhamini maslahi ya utawala wa Kizayuni katika eneo kwa kutenda jinai kadhaa za kinyama, ikiwa ni pamoja na za mauaji ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran na makamanda wa Muqawama.

Mohsen Fakhrizadeh, Majid Shahryari, Masoud Ali Mohamadi, Daryush Rezai Nejad, Mostafa Ahmadi Roushan na Reza Qashqai ni miongoni mwa wanasayansi wa nishati ya nyuklia wa Iran waliouliwa shahidi katika miaka ya karibuni na vibaraka na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD.

Luteni Jenerali Qasem Suleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC naye pia aliuliwa shahidi tarehe 3 Januari 2020 katika shambulio la kigaidi lililofanywa na jeshi la anga la Marekani, wakati akiwa pamoja na aliyekuwa naibu mkuu wa harakati ya Hashdu-Sha'abi, Abu Mahdi al Muhandis karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, Iraq, alipoelekea nchini humo kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo.

Lengo kuu la maadui la kufanya hujuma hizo za kigaidi ni kuzuia nguvu na ushawishi unaoongezeka kila uchao wa Iran na vilevile kukwamisha mpango wa taifa hili wa kunufaika na teknolojia na nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani. Katika makala yake moja ya uchambuzi liliyoandika baada ya kuuawa mwanasayansi mbobezi wa nyuklia wa Iran Mohsen Fakhrizadeh mnamo Novemba 2020, gazeti la Independent lilieleza yafuatayo: "Mauaji ya karibuni nchini Iran ni sehemu ya juhudi zisizo na mwisho za taasisi ya intelijensia ya Israel ikishirikiana na taasisi wenza za Magharibi ikiwemo MI6 na CIA za kujaribu kuvuruga, kuchelewesha na au kama itawezekana kuizuia kikamilifu Iran isiweze kufikia lengo lake la kumiliki teknolojia ya nyuklia."

Kwa sababu ya hayo, hata kama viongozi wa utawala wa Kizayuni, kama ilivyokuwa huko nyuma, hawajakiri hadharani kuhusika utawala huo na mauaji ya Sayyad Khodaei, lakini kwa kuzingatia majukumu aliyokuwa akitekeleza Shahidi huyo ya ulinzi wa Haram nchini Syria kuna kila sababu ya kuwafanya Wazayuni watuhumiwa nambari moja wa jinai hiyo.

Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanadhani kuwa kwa kufanya jinai za aina hiyo za kigaidi wataweza kuzuia malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu yasifikiwe; lakini wananchi wa Iran wameshaonyesha kila mara kuwa ni waendelezaji wa njia ya Mashahidi; na damu za Mashahidi ndizo zinazodhamini utukukaji wa Iran ya Kiislamu.

Kushoto: Shahidi Hassan Sayyad Khodaei. Kulia: eneo la tukio aliposhambuliwa ndani ya gari mbele ya nyumba yake

Pamoja na yote hayo lililowazi ni kwamba, jinai hii ya maadui, ambayo imenyamaziwa kimya na kuungwa mkono na nchi zinazodai kuwa zinapambana na ugaidi, katu haitaachwa bila kujibiwa; na kama alivyosisitiza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kisasi cha damu ya Shahidi Khodaei kitawaandama tu waliotenda jinai hiyo.../