May 23, 2022 15:08 UTC
  • Iran na Oman zatiliana saini hati 12 za kustawisha ushirikiano + Video

Leo Jumatatu, Rais Ebrahim Raisi amefanya ziara rasmi ya siku moja nchini Oman na kupokewa kwa heshima zote na Sultan Haitham bin Tariq wa nchi hiyo.

Miongoni mwa matunda ya ziara hiyo rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Oman ni kutiwa saini hati 12 za kustawisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili ndugu.

Ziara ya Oman ni ya 5 kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu alipoingia madarakani miezi tisa iliyopita. Msafara wa Rais Ebrahim Raisi huko Oman una mawaziri na manaibu mawaziri 50 pamoja na wakurugenzi wa ngazi za juu wa masuala ya biashara wa Iran. 

Mwaka jana, Iran na Oman zilikuwa na mabadilishano ya kibiashara yenye thamani ya dola bilioni 1.3. Sasa hivi nchi hizo mbili zinafanya juhudi za kuhakikisha mabadilishano hayo yanatanua wigo wake hadi katika masuala tofauti ya kiuchumi na kutumia vizuri zaidi fursa za uwekezaji kwa shabaha ya kuongeza zaidi na zaidi kiwango cha mabadilishano yao ya kibiashara.

Akizungumza kabla ya kuondoka uwanja wa ndege wa Tehran kuelekea Muscat mapema leo asubuhi, Rais wa Iran amesema safari yake nchini Oman inafanyika kwa msingi wa kuimarisha ujirani mwema. Amesema mazungumzo yake na wakuu wa Oman yatahusu kustawisha uhusiano wa pande mbili na pia wa kieneo.

Rais Raisi ameongeza kuwa ameelekea Oman kufuatia mwaliko rasmi wa Sultan Haitham bin Tariq Al Said na kuongeza kuwa kuna uhusiano wa kirafiki na kidugu baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman.