May 24, 2022 01:18 UTC
  • Iran na Afrika Kusini zitilia mkazo wajibu wa kustawishwa uhusiano baina yao

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa ametilia mkazo wajibu wa kuimarishwa ushirikiano baina ya nchi yake na Afrika Kusini na kusisitiza kuwa, kutiwa nguvu ushirikiano baina ya Tehran na Pretoria ni jambo la dharura sana kwa ajili ya kupambana na fikra potofu ya kila nchi kujikumbizia mambo yote upande wake.

Ali Bagheri Kani alisema hayo jana (Jumatatu) wakati alipoonana na Bi Candith Mashego-Dlamini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini hapa Tehran na kuongeza kuwa, nafasi muhimu ya Iran na Afrika Kusini katika masuala ya kieneo na kimataifa haihatarishi manufaa ya taifa lolote linalonyongeshwa. Amesema, ushirikiano wa nchi hizi mbili umesimama juu ya msingi wa siasa za kuleta utulivu, usalama, amani na uadilifu kieneo na kimataifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesema, ushirikiano wa Iran na Afrika Kusini haupaswi kuishia kwenye kudhamini mahitaji ya muda mfupi tu bali unapaswa uwe na mikakati ya muda mrefu na uguse sekta zote.

Kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ni katika ajenda kuu za Iran

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Candith Mashego-Dlamini amegusia jinsi janga la UVIKO-19 yaani corona lilivyoziathiri vibaya nchi za dunia katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na namna walimwengu walivyozidi kuona ukosefu mkubwa wa uadilifu katika mahusiano ya kimataifa na kuongeza kuwa, kuna udharura wa kutiwa kasi uhusiano wa Tehran na Pretoria katika nyuga mpya hususan ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kimataifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini yuko hapa Tehran akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa nchi yake kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha 10 cha kamati ya pamoja ya mashauriano ya kisiasa ya wizara za mambo ya nje za Iran na Afrika Kusini.

Tags