May 24, 2022 11:06 UTC
  • Iran yalaani hatua ya jamii ya kimataifa ya kupuuza jinai za utawala wa Kizayuni

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani namna jamii ya kimataifa inavyopuuza jinai za kukaririwa za utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema jambo hilo limeufanya utawala huo upate kiburi zaidi cha kuendeleza jinai na uchokozi.

Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Upuuzaji wa jamii ya kimataifa kuhusu uvamizi wa mara kwa mara na utawala wa Kizayuni, unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu, dhidi ya Syria sambamba na ukiukwaji wa wazi wa sheria na mikataba ya kimataifa ni jambo ambalo limepelekea viongozi wa utawala huo kuthubutu zaidi na kutojizuia kutenda jinai."

Aidha amesema: "Uungaji mkono wa wazi na wa siri wa utawala wa Mareknai ni nukta muhimu ambayo imepelekea utawala ghasibu wa Kizayuni kupata uthubutu wa kutenda jinai ambapo sasa si tu kuwa utawala huo unaendelea kukalia kwa mabavu Miinuko ya Golan ya Syria, bali pia mara kwa mara hutekeleza mashambulizi ya kijeshi kwa makombora na kwa ndege za kivita dhidi ya watu wa Syria na miundo msingi ya nchi hiyo."

Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel

Khatibzadeh amesema katika miaka ya hivi karibuni ya mgogoro wa Syria, Jeshi la Anga la Israel limekuwa na nafasi kubwa katika kuunga mkono magaidi nchini Syria kwani kila wakati magaidi wanaposhindwa na Jeshi la Syria na waitifaki wake, ndege za kivita za Israel hutekeleza mashambulizi ya haraka dhidi ya jeshi hilo.

Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vitendo hivyo vya kivamizi vya utawala wa Kizayuni na inasisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za kivitendo kukabiliana na uchokozi huo na kuongeza kuwa, hatua hizo za kuwajibu Wazayuni zinapaswa kuchukuliwa katika medani ya kivita na pia katika duru za kimataifa.