May 24, 2022 11:18 UTC
  • Jenerali Salami: Uchokozi wowote wa adui dhidi ya Iran utakabiliwa na jibu kali

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema damu ya Shahidi Hassan Sayyad Khodaei haitamwagika bure na kusisitiza kuwa, hatua na uchokozi wowote wa adui utakabiliwa na jibu kali.

Mlinzi wa Haram, Kanali Hassan Sayyad Khodaei aliuawa shahidi Jumapili mjini Tehran katika hujuma ya kigaidi ya wapinga Mapinduzi ya Kiislamu na maajenti wa madola ya kiistikbari duniani.

Mazishi ya Shahid Hassan Sayyad Khodaei yamefanyika leo mjini Tehran na kuhudhuria na halaiki kubwa ya watu katika Medani ya Imam Hussein AS.

Akizungumza na Kanali ya Televisheni ya Al Masirah, Brigedia Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema damu ya Shahidi Khodaei haitamwagika bure na kwamba jibu kali litatolewa kuhusu jinai hiyo.

Brigedia Jenerali Salami amesema Iran haitamuacha adui abakie hivi hivi na kwamba uchokozi wa adui utakabiliwa na jibu kali

Msafara wa mazishi ya Shahidi  Kanali Hassan Sayyad Khodaei

Jana pia Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitoa taarifa kuhusu mauaji ya mmoja wa askari wake, Shahidi Khodaei, na kusema maadui kwa mara nyingine tena wamedhihirisha dhati ya shari yao kwa ugaidi.

Msemaji wa IRGC amesisitiza kuwa, makundi ya kigaidi yenye mfungamano na uistikbari na Uzayuni wa kimataifa yatalipa gharama kwa jinai zao.

Brigedia Jenerali Ramezan Sharif, msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu  ameeleza kuwa, kuuawa shahidi Kanali Hassan Sayyad Khodaei kutaongeza azma ya IRGC ya kulinda usalama, mamlaka ya kujitawala na maslahi ya kitaifa sambamba na kukabiliana na maadui wa taifa la Iran.