May 25, 2022 03:32 UTC
  • Iran yasambaratisha genge la magendo ya silaha kusini mashariki mwa nchi

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi la mkoa wa Sistan va Balichustan ametangaza habari ya kusambaratishwa genge la magendo ya silaha kwenye mkoa huo wa kusini mashariki mwa Iran.

Kanali Morteza Jokar ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, maafisa wa polisi wa wilaya ya Hirman wamefanikiwa kukusanya taarifa za uhakika za kupenyezwa kimagendo silaha za kivita na za uwindaji ndani ya ardhi ya Iran zikiwa zimefichwa kwa utaalamu wa hali ya juu kwenye lori moja lililokuwa linapita tu nchini Iran kuelekea nchi nyingine.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kikosi kazi cha jeshi la polisi kilianza kufuatilia kwa kina taarifa hizo na kufanikiwa kusambaratisha genge hatari la magendo ya silaha kusini mashariki mwa Iran.

Kanali Morteza Jokar ameongeza kuwa, uchunguzi wa maafisa wa jeshi la polisi la wilaya ya Hirman ya mkoa wa Sistan Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran umethibitisha kuwa, silaha hizo zimepelekwa kwa watu wawili ambao ni maarufu kwa magendo ya silaha katika kijiji kimoja cha wilaya ya Hirman.

Kaimu huyo wa Mkuu wa Jeshi la Polisi la mkoa wa Sistan va Baluchistan ameongeza kuwa, maafisa wa jeshi la polisi la Iran walilikamata lori hilo, wakamtia mbaroni dereva wake pamoja na wafanya magendo hao wawili wa silaha. Silaha 9 za kivita na uwindaji zimekamatwa kwenye nyumba ya wafanya magendo hao.