May 26, 2022 11:04 UTC
  • Iran: Tuna nia ya kweli ya kufikia mapatano imara na madhubuti ya nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran ina ni ya kweli ya kufikia makubaliano yenye nguvu na madhubuti ya nyuklia katika mazungumzo ya mjini Vienna Austria.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo leo (Alkhamisi) pembeni mwa kikao cha Davos wakati alipohojiwa na televisheni ya CNN ya Marekani na kuongeza kuwa, hivi karibuni Iran ilikuja na ubunifu mpya wa kufufua makubaliano ya nyuklia na kwamba rais wa Marekani Joe Biden anapaswa kuachana na siasa za vikwazo vya kiwango cha juu.

Amesema, kurejea kwenye mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 kuna uhusiano wa moja kwa moja na kurejea Iran katika shughuli zake za kiuchumi kimataifa.

Marekani inaendeleza vikwazo dhidi ya Iran katika hali ambayo viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali ya Joe Biden wamekuwa wakikosoa siasa za vikwazo vya kiwango cha juu za rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump katika nyakati na minasaba tofauti lakini kwa maneno matupu.

Mazungumzo ya Vienna ya kufufuta JCPOA

 

Wataalamu wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, kuendelea vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran wakati huu wa mazungumzo ya kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA hakuna tafsiri nyingine isipokuwa kuendeleza uadui na uistikbari wa miongo mingi wa serikali mbalimbali zinazoingia madarakani huko Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kuwa, hivi sasa tunachokiona ni hatua za kiwendawazimu za uraibu wa Marekani wa kuweka vikwazo kiasi kwamba hata wakati huu wa mazungumzo, Washington inaendelea kuiwekea Iran vikwazo.