May 27, 2022 02:23 UTC
  • Iran yakosoa mitazamo ya upande mmoja na taathira zake hasi kwa utulivu wa eneo na usalama wa kimataifa

Awamu ya tatu ya mazungumzo ya kisiasa kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Italia ilifanyika siku ya Jumanne mjini Tehran, chini ya uenyekiti wa Ali Bagheri, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa na Ettore Plato, Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia.

Katika kikao hicho Ali Bagheri mbali na kueleza kuwa, uthabiti na usalama wa baadaye wa dunia hautapatikana kupitia mitazamo ya upande mmoja wala njia za kijeshi, amesema: "Hali na vitisho vya kimataifa vinapasa kushughulikiwa kupitia mashauriano endelevu na ushirikiano wa kudumu kati ya Iran na Ulaya.

Matamshi ya afisa huyo wa ngazi ya juu wa Iran yamelenga siasa za mabavu na za upande mmoja za Marekani ambayo katika miongo miwili iliyopita ilianzisha vita vya kieneo ikiwemo kuikalia kwa mabavu Iraq na Afghanistan na pia kuingilia Syria kwa manufaa ya makundi ya kigaidi yanayolenga kuipindua serikali halali ya nchi hiyo. Jambo hilo bila shaka limevuruga uthabiti na ualama wa kieneo na kuimarisha makundi ya kigaidi katika eneo zima la Asia Magharibi. Washington, hasa katika kipindi cha utawala wa Donald Trump, ilienda mbali zaidi na kuyumbisha makabiliano ya kisiasa na kibiashara sio tu na wapinzani wa Amerika kama vile Uchina bali pia na washirika wake wa Ulaya, na hivyo kuvuruga pakubwa muungano wa ushirikiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantiki kati ya Ulaya na Marekani.

Ingawa Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden amejaribu kurekebisha uhusiano huo, lakini ni wazi kuwa matukio ya hivi karibuni, hasa msimamo wa Marekani kuhusu vita vya Ukraine, yanaonyesha kwamba Washington bado inaitaka Ulaya ifuate siasa zake bila kusita, hata katika masuala muhimu yanayoigusa Ulaya moja kwa moja kama vile vikwazo vya nishati dhidi ya Russia, jambo ambalo bila shaka litakuwa na madhara makubwa kwa nchi za Ulaya.

Ali Bagheri

Hii inaonyesha wazi kuwa Marekani bado haijaachana na mitazamo yake ya upande mmoja kuhusu masuala muhimu ya kimataifa na ingali inazishinikiza nchi nyingine za dunia zitii na kufuata mitazamo yake hiyo ya kimaslahi bila kuuliza maswali. Hii ni katika hali ambayo Wazungu wanapasa kubuni sheria na kuchukua misimamo kwa msingi wa malengo na maslahi yao ya kitaifa. Suala hilo limezingatiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mazungumzo ya Tehran. Huku akiashria kuwa kuna mambo mengi muhimu ambayo yanatoa udharura wa kuimarishwa uhusiano wa Iran na Ulaya, Bagheri amesisitiza kuwa, kuna uchochezi wa kigeni hususan kutoka upande ule mwingine wa bahari ya Atlantiki ambao daima unafuatilia kuharibu na kuyumbisha uhusiano huo, hivyo kuna haja ya pande mbili hizi kufanya kila linalowezekana kwa ajili ya kuulinda usiharibiwe na  maadui. Matamshi hayo ya Bagheri yanakusudia juhudi zisizokoma za Marekani za kujaribu kuiweka Ulaya mbali na Iran na kuishawishi ishirikiane nayo katika kuchukua misimamo ya chuki na uhasama dhidi ya Iran.

Katika hali ambayo misimamo ya Ulaya kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanaonyesha wazi kuwa Ulaya inataka kuyafufua kwa maslahi yake, lakini Washington licha ya mazungumzo ya muda mrefu yanayoendelea huko Vienna Austria, inaendelea kusisitiza juu ya kutekelezwa misimamo yake wa upande mmoja na kuendelea kuishinikiza Iran itii matakwa yake. Hii ni katika hali ambayo Tehran imetangaza wazi na wakati huo huo kuwaonya Wazungu kwamba haiko tayari kurejea katika utekelezaji wa majukumu yake katika mapatano ya JCPOA iwapo haitaondolewa vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa na Marekani, pamoja na kutolewa dhamana kwamba nchi hiyo haitajitoa tena katika mapatano hayo ya kimataifa.

Suala jingine lililozungumziwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mashauriano yake na upande wa Italia ni kuhusu hali tata ya kimataifa na vitisho muhimu vinavyotokana na vita vya Ukraine, na hasa kuhusu suala zima la nishati na usalama wa chakula kimataifa, hususan barani Ulaya. Tehran inaona kwamba changamoto hiyo inaweza kutatuliwa kupitia mashauriano endelevu kati ya Iran na Ulaya.

Mazungumzo ya JCPOA mjini Vienna, Austria

Naibu Waziri huyo pia ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kivitendo kwa ajili ya kusaidia kuleta amani na utulivu katika nchi za Afghanistan na Yemen, kwa msingi  wa mashauriano na ushirikiano ambao umekuwepo kati ya pande mbili hizo. Na hasa kwa kuzingatia kushindwa na kuondoka kwa madhila askari wa Marekani na Nato huko Afghanistan kutokana na kung'ang'ania siasa za upande mmoja kuhusu masuala muhimu ya kimataifa. Ali Bagheri anasema: "Somo muhimu zaidi la kimkakati tunalojifunza kutokana na historia ya miaka ishirini iliyopita ya eneo letu ni utendaji (mbovu) wa nchi za Magharibi na NATO nchini Afghanistan. Suala hilo pekee linathibitisha wazi kwamba uthabiti na usalama wa baadaye wa dunia hautadhaminiwa kupitia siasa za upande mmoja wala njia za kijeshi."

Tags