May 27, 2022 02:33 UTC
  • Kiongozi Muadhamu atoa mkono wa pole kufuatia ajali ya kuporomoka jengo Abadan

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa salamu za rambirambi kufuatia ajali ya kuporomoka jengo la ghorofa katika mji wa Abadan, makao makuu wa mkoa wa Khuzestan wa kusini magharibi mwa Iran.

Katika ujumbe wake huo wa tanzia, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei mbali na kuelezea masikitiko yake makubwa kutokana na watu waliopoteza maisha na kujeruhiwa kwenye ajali hiyo, ameagiza kuongezwa kasi ya uokoaji ili kupunguza maafa na vile vile kufuatiliwa kwa haraka waliofanya uzembe wa kutokea ajali hiyo waweze kuhukumiwa ipasavyo na kuwa funzo kwa wengine ili makosa kama hayo yasitokee tena.

Katika ujumbe wake huo uliosomwa jana jioni kwenye kikao cha dharura kilichoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kufuatilia ripoti za karibuni kabisa za ajaili hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema:

Kifusi cha jengo la ghorofa lililoporomoka Abadan

 

Bismillahir Rahmanir Rahim

Tukio la kusikitisha la Abadan, mbali na kuhitajia hatua za haraka na kutumiwa uwezo wote uliopo ili kupunguza madhara ambapo kwa sasa hivi ndilo jambo muhimu zaidi, linahitajia pia ufuatiliaji wa kisheria kwa kushirikiana na Idara ya Mahakama ili waliofanya uzembe wa kutokea tukio hilo waweze kupewa adhabu ambayo itakuwa funzo kwa wengine. Vile vile ajali hiyo inatuwajibisha viongozi wote humu nchini kufanya juhudi kubwa za kuzuia kutokea tena matukio kama hayo katika kona zote za Iran. Ni lazima kwangu kuwashukuru maafisa wa serikali kwa kazi yao waliyoifanya katika kipindi cha siku kadhaa sasa na ninaagiza kuweko ufuatiliaji kamili na wa nguvu zote wa suala hilo. Ninatoa mkono wa pole kwa wote waathiriwa wa tukio hilo na ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu subira na malipo mema. Sayyid Ali Khamenei.

Jumatatu wiki hii, sehemu moja ya jengo la ghorofa 10 la kibiashara liliporomoka huko Abadan, makao makuu wa mkoa wa Khuzestan wa kusini magharibi mwa Iran na kupelekea watu wasiopungua 19 kupoteza maisha na zaidi ya 30 wengine kujeruhiwa.