May 27, 2022 06:59 UTC
  • Shamkhani: Dunia iungane kupambana na ubeberu wa Marekani kwa pande zote

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, dunia inapaswa kuungana katika kupambana na siasa za kibeberu za Marekani za kujikumbizia kila kitu upande wake.

Shirika la habari la Iran Press limetangaza habari hiyo leo Ijumaa na kumnukuu Ali Shamkhani akisema hayo huko Tajikistan anakoshiriki mazungumzo ya nne ya usalama wa kieneo na kuongeza kuwa, kuna udharura wa kutiwa nguvu kadiri inavyowezekana ushirikiano wa Iran na nchi kama Russia katika matukio ya hivi sasa ya kimataifa.

Aidha amesema katika mazungumzo yake na Nikolai Patrushev Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapambana na vikwazo na mashinikizo makubwa ya nchi za kibeberu hasa Marekani kwa miaka 43 sasa na hivi sasa taifa la Iran limekuwa nembo ya kusambaratisha vikwazo za madola ya kiistikbari.

Bendera za Iran na Russia

 

 

Vile vile ameelezea wajibu wa kufuatiliwa na kutekelezwa kivitendo ushirikiano wa kiistratijia wa Tehran - Moscow kwa ajili ya kupambana na siasa za Marekani za kupenda makuu na kujikumbizia kila kitu upande wake. Amesema: Kuandaa mazingira mazuri ya ushirikiano katika wakati huu wa vikwazo na kubadilisha vikwazo hivyo kuwa fursa za kuimarisha uchumi na kutegemea bidhaa za ndani ya nchi ni jambo la dharura.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran pia ameelezea kusikitishwa na hali ya wananchi wa Afghanistan na jinai zinazofanywa na magenge ya kigaidi nchini humo na kuongeza kuwa, kuundwa serikali inayoshirikisha watu wote na kuondoa mashinikizo ya kimaisha ya wananchi ni miongoni mwa njia bora za kuwapunguzia masaibu wananchi Waislamu wa Afghanistan.

Tags