May 28, 2022 02:43 UTC
  • Shamkhani: Iran na Russia zishirikiane kukabiliana na Marekani

Afisa wa ngazi ya juu wa usalama wa Iran amekosoa vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia kuhusu mgogoro wa Ukraine, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuungana na kusimama dhidi ya sera za upande mmoja za Washington.

Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) akiwa katika kikao na mwenzake wa Russia Nikolai Patrushev kando ya mkutano wa nne wa Mazungumzo ya Usalama wa Kieneo katika mji mkuu wa Tajikistan, Dushanbe siku ya Ijumaa alitoa wito wa kupinga sera za upande mmoja (unilateralism) za Marekani.

“Ulimwengu lazima uungane dhidi ya sera za upande mmoja za Marekani. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa chini ya vikwazo kwa muda wa miaka 43 iliyopita, na imekuwa kielelezo cha kutofaulu kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi huru," alisema.

Amesisitiza ulazima wa kuwepo ushirikiano wa kistratijia kati ya Tehran na Moscow katika kukabiliana na siasa za upande mmoja za Marekani.

"Inaonekana kana kwamba vikwazo dhidi ya Russia havitaondolewa mara baada ya vita vya [Ukraine] kumalizika. Kwa hiyo, ni muhimu kubuni mfumo madhubuti wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi zilizowekewa vikwazo,” Shamkhani alisema.

Mapigano nchini Ukraine

Patrushev, kwa upande wake, alisema vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia vingetekelezwa hata kama mgogoro wa Ukraine usingezuka.

Aidha amesema vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia vimewafanya wananchi watambue kuwa haifai kutegemea nchi za Magharibi. Ameongeza kuwa kutegemea nchi za Magharibi kulikuwa kumekandamiza uwezo wa viwanda vya Russia vinavyozalisha bidhaa mbali mbali kitaifa.

Aidha amesema oparesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine ilifichua mpango wa Marekani wa kuendeleza maabara za silaha za kemikali na kibaolojia katika nchi hiyo, akisisitiza kwamba Moscow inapanga kuchapisha ripoti muhimu kuhusu kadhia hiyo katika siku za usoni.