May 28, 2022 03:15 UTC
  • IRGC: Meli mbili za mafuta za Ugiriki zimekamatwa katika maji ya Ghuba ya Uajemi kwa kukiuka taratibu

Idara Kuu ya Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imetangaza kuwa meli mbili za mafuta za Ugiriki zimekamatwa katika maji ya Ghuba ya Uajemi kwa sababu ya kukiuka taratibu.

Taarifa iliyotolewa na Idara Kuu ya Mahusiano ya Umma ya IRGC imebainisha kuwa kikosi cha wanamaji cha jeshi hilo, jana kilizikamata meli mbili za mafuta za Ugiriki katika maji ya eneo la Ghuba ya Uajemi kutokana na kukiuka taratibu. Hatua hiyo imechukuliwa na Iran baada ya balozi mdogo wa Ugiriki mjini Tehran kuitwa Wizara ya Mambo ya Nje na agizo alilopewa la kuitaka nchi yake iache kufanya vitendo vya uharamia.

Mwezi uliopita, Ugiriki iliikamata meli moja ya mafuta iliyokuwa na bendera ya Iran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ugiriki iliipatia Marekani shehena ya mafuta iliyokuwemo kwenye meli hiyo.

Kufuatia kukamatwa shehena iliyokuwemo kwenye meli iliyokuwa na bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la maji ya Ugiriki, balozi mdogo wa nchi hiyo hapa Tehran aliitwa wizara ya mambo ya nje na kubainishiwa malalamiko makali ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya hatua hiyo.

Jana hiyohiyo, balozi mdogo wa Uswisi hapa Tehran ambao ndio unaohusika na maslahi ya Marekani, aliitwa wizara ya mambo ya nje na kubainishiwa wasiwasi na malalamiko makali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na kuendelea ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa zinazohusu haki za baharini na mikataba ya kimataifa hususan inayohusu uhuru wa vyombo vya majini na biashara huru za kimataifa na kusisitiziwa ulazima wa kuachiwa huru meli ya Iran iliyokamatwa pamoja na shehena yake.../

Tags