May 28, 2022 10:13 UTC
  • Rais wa Iran atuma salamu za pongezi kwa mnasaba wa Siku ya Taifa la Ethiopia

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe wa kheri na fanaka kwa serikali na watu wa Ethiopia kwa mnasaba wa kuwadia siku ya kitaifa ya nchi hiyo.

Katika ujumbe wake huo leo Jumamosi, Rais Ebrahim Raisi amemtumia salamu za pongezi Rais Bi. Sahle-Work Zewede wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia.

Rais Raisi amempongeza rais na watu wa Ethiopia kwa mnasaba wa siku ya kitaifa ya nchi hiyo na kuelezea matumaini kuwa, uhusiano wa kidugu baina ya Iran na Ethiopia utaendelea kwa msingi wa kuheshimiana pande mbili. Aidha ameelezea matumaini kuwa uhusiano wa Iran na Ethiopia utazidi kuimarika na utakuwa ni wenye manufaa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatekeleza sera za kuwa na uhusiano mwema na mataifa yote duniani ambapo bara la Afrika linapewa kipaumbele katika sera za kigeni za Tehran. 

Wananchi wa Ethiopia huadhimisha Siku ya Kitaifa ambayo hujulikana pia kama Siku ya Kuangushwa Utawala wa Derg. Siku hii huadhimishwa kila mwaka Mei 28 kukumbuka wakati utawala wa kiimla wa Kikomunisti wa Derg ulipoangushwa kufuatia mapambano ya muda mrefu ya wananchi.