May 28, 2022 10:23 UTC
  • Umoja wa Waislamu utapelekea kuundwa umma wa Kiislamu wenye nguvu

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema umoja wa Waislamu utapelekea kuibuka umma wa Kiislamu wenye nguvu za kukabiliana na madola makubwa ya kibebberu na kiistikbari.

Akizungumza katika mkutano mjini Tehran na ujumbe wa wanazuoni kutoka Nepal, Hujjatul Islam Hamid Shahriari amesema umoja wa Waislamu utapelekea kuundwa Umma wa Kiislamu wenye nguvu ambao utaweza kusimama kidete mbele ya mdola ya kibeberu na kiistikbari.

Amesema ujumbe muhimu zaidi wa Hayati Imam Khomeini MA ulikuwa ni kukabiliana na madola ya kiistikbari na kuwasaidia wanaodhulumiwa katika nchi za Kiislamu,

Hujjatul Islam Shahriari amesema katika karne mbili zilizopita, madola ya kiistikbari, kinara wao akiwa ni Marekani, yamejaribu sana kueneza sera za uliberali duniani.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ameendelea kusema kuwa, kuarifisha thamani na mafundisho ya Kiislamu kwa umma ndiyo njia ya kufikia ustawi na saada na kusema hilo ni jukumu la maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu. Aidha amesema Waislamu wa madhehebu zote wana nukta za pamoja katika mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Sunna ya Mtume Muhammad SAW.

Hali kadhalika amesema tafauti kubwa zaidi ya mtindo wa Kiislamu wa maisha na mtindo wa maisha wa Kimagharibi ni uzingatiwaji mipaka ya Mwenyezi Mungu.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha pamoja Madhehebu za Kiislamu, yenye makao yake mjini Tehran, amesema madola ya Magharibi yanataka Waislamu waachane na mfumo wa Kiislamu wa maisha na wafuate uliberali na mbinu wanayotumia kufikia lengo lao hilo ni kuibua mifarakano katika Umma wa Kiislamu.