May 29, 2022 03:55 UTC

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limezindua kituo kipya cha siri kilicho chini ya ardhi chenye idadi kubwa ya ndege za kisasa za kivita zisizo na rubani.

Kituo hicho  ambacho kimepewa jina la Kituo cha Kistratijia cha 313 cha Ndege Zisizo na Rubani  kimezinduliwa Jumamosi na Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri ambaye amekagua zana za kisiasa za kivita zilizo katika kituo hicho.

Aidha Jumamosi  Jeshi la Iran  pia lilizindua kombora la cruise lijulikanalo kama Heidar 1 lenye uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 200 kwa kasi ya kilomita 1000 kwa saa. Kombora la Heidar 1 linaweza kuvurumishwa kutoka katika ndege isiyo na rubani. Jeshi la Iran pia limezindua kombora jingine lijuliknalo kama Heidar 2 ambalo linaweza kuvurumishwa kutoka katika helikopta.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema Iran kamwe haidunishi vitisho vya maadui na daima iko katika hali ya tahadhari.

Aidha amesema ndege zisizo na rubani au drone ni muhimu sana katika mapigano ya kisasa na kuongeza kuwa Jeshi la Iran lina ufahamu wa kina kuhusu zana zinazohitajika katika vita vya mustakabali na hivyo limejizatiti kwa silaha za kisasa kabisa sambamba na kubuni mbinu mpya za kivita.

Kituo cha siri cha Jeshi la Iran cha ndege za kivita zisizo na rubani  kilicho chini ya ardhi

Amesema hivi sasa ndege zisizo na rubani ni muhimu sana katika oparesheni za kijeshi za kujihami na zinatumiwa na majeshi ya nchi kavu, anga, majini na hali kadhalika katika oparesheni za upelelezi na vita vya kieletroniki pamoja na kazi zingine nyingi.

Baqeri amesema hivi sasa Iran imejitosheleza kikamilifu katika uundaji wa ndege zisizo na rubani.

Naye Kamanda wa Jeshi la Iran Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi amesema jeshi limeonyesha umma sehemu ndogo tu ya uwezo wake wa ndege za kivita zisizo na rubani na kuongeza kuwa jitihada za Iran za kuimarisha uwezo wake wa kivita, ukiwemo wa ndege zisizo na rubani, haziwezi kusimamishwa.

Hii hapa ni klipu ya mwandishi habari wa Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB) aliyepata fursa ya kufika katika kituo hicho cha siri cha ndege zisizo na rubani.

 

Tags