Jun 01, 2022 08:07 UTC
  • Rais Raisi: Kuipa umuhimu Afrika ni moja ya mihimili mikuu ya sera za nje za Iran

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuipa umuhimu Afrika ni moja ya mihimili mikuu ya sera za nje za Tehran.

Rais Raisi ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Rais Macky Sall wa Senegal ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU).

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa pongezi kwa watu wa bara la Afrika na taifa la Senegal kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Taifa ya Afrika na akaashiria mchango wa Umoja wa Afrika katika kukabiliana na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na vikwazo vya Ukoloni na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na itaendelea kuwa mshirika wa kuaminika kwa mataifa yote ya Afrika.

Seyyid Ebrahim Raisi amegusia pia uwezo wa kiwango cha juu wa kitaalamu na kiufundi ilionao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akabainisha kuwa Tehran na Dakar zina uhusiano mzuri baina yao lakini kiwango cha sasa hakiridhishi na inapasa kiongezwe zaidi hadi upeo unaostahiki.

Amesisitiza kuwa Iran iko tayari kikamilifu kupanua na kustawisha uhusiano wake na nchi za bara la Afrika na hasa Senegal na kustawisha uhusiano wa Kusini - Kusini na hakuna mpaka wowote juu ya suala hilo.

Kwa upande wake, Rais Macky Sall wa Senegal ameashiria uhusiano wa kirafiki wa Iran na nchi za Afrika ikiwemo Senegal na akasema, nchi yake iko tayari kutoa kila ushirikiano kwa ajili ya kustawisha mashirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Aidha ameongeza kuwa, kuna ushirikiano mzuri  baina ya mashirika ya Senegal na baadhi ya mashirika ya Iran.../ 

Tags